visit here again on mukebez.blogspot.com


CHANGE YOUR LIFE

CHANGE YOUR LIFE
Go to Amazon .com and get the copy of this book to make your life better.

Jumatano, 23 Aprili 2014

WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA JIBUNI HAYA MASWALI YA JAJI WARIOBA.


Dar es Salaam.Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ameuliza maswali saba ya msingi kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wanaopinga Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume yake akitaka wawajibu wananchi ili kutuliza kiu yao.
Jaji Warioba ambaye tangu awasilishe Rasimu ya Katiba Desemba 30, mwaka jana amegeuka kuwa adui kwa watu wanaotaka muundo wa serikali mbili, aliuliza maswali hayo jana katika uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza kuhusu mchakato wa Katiba.
Akizungumza kwa ukali, Jaji Warioba alisema: “Kwanza, jibuni kwa nini mnapinga muundo wa Muungano wakati walioupendekeza ni wananchi?
“Sheria inasema uwepo wa Muungano na mapendekezo katika rasimu hayasemi Muungano usiwepo. Kumbukeni kuwa wananchi walitakiwa kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha Muungano.”
Katika swali lake la pili, Warioba alisema kwa nini Tanganyika imevaa koti la Muungano? Kwa kuwa katika ukusanyaji wa maoni wananchi walieleza kuwa Serikali ya Muungano ya sasa siyo ya Muungano, ni ya Tanganyika.
Katika swali la tatu alisema wajumbe hao wanatakiwa kujibu maelezo ya wananchi ambao waliieleza tume hiyo kuwa Katiba imevunjwa na madaraka ya rais yamechukuliwa na sasa kuna marais wawili katika nchi moja.
“Tume inapewa lawama kubwa, wajibuni wananchi hii tume ilitumwa na nani kukusanya maoni ya wananchi? Waambieni ilikusanya maoni hayo kwa kutumia sheria ipi zaidi ya ile ya Mabadiliko ya Katiba?” alisema Jaji Warioba katika swali lake la nne.
Katika swali lake la tano, Warioba aliwataka wajumbe hao kutoa sababu za kumtuhumu kuwa amependekeza muundo wa serikali tatu kwa sababu yeye pamoja na (Joseph Butiku) walikuwa wajumbe wa Tume ya Jaji Kisanga na Jaji Nyalali ambazo nazo zilipendekeza muundo wa serikali tatu, kitu ambacho alisema si kweli na hawakuwahi kuwa mjumbe wa tume hizo.
Pia, aliwataka wajumbe hao kujibu swali la sita, kwa nini hawataki kuzungumzia yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na badala yake wanageuza rasimu hiyo kuwa imeandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Katika swali lake la saba, aliwataka wajumbe kujibu kwa nini wanaishutumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa imeingiza maoni yake, wakati ilikusanya maoni hayo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba?
Alisema badala ya kujadili hoja za msingi, wajumbe wa Bunge hilo wamekuwa wakitoa lugha za kejeli na matusi kwa baadhi ya watu (akiwamo na yeye), kitendo ambacho alisema si sahihi na kinaweza kuligawa taifa kwa sababu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba yametokana na maoni ya wananchi.
Katika uzinduzi huo walikuwepo baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo ambao ni Dk Hamisi Kigwangalla aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Julius Mtatiro, Maria Sarungi na aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole.KUTOKA MWANANCHI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni