visit here again on mukebez.blogspot.com


CHANGE YOUR LIFE

CHANGE YOUR LIFE
Go to Amazon .com and get the copy of this book to make your life better.

Jumatatu, 28 Aprili 2014

UTEKELEZAJI WA MABADILIKO YA MATUMIZI YA BARABARA DAR KUANZA LEO.

Dar es Salaam.Utekelezaji wa mabadiliko ya matumizi ya barabara katikati ya Jiji la Dar es Salaam unaanza leo na alama za kuonyesha njia hizo zimeshawekwa katika barabara zote zitakazohusika.
Mabadiliko makubwa yanafanywa katika Barabara za Samora na Sokoine. Barabara ya Samora sasa itakuwa inatoka badala ya kuingia katikati ya jiji kama ilivyokuwa na ile ya Sokoine itakuwa inaingia tu badala ya kuingia na kutoka katikati ya jiji.
Akizungumzia mabadiliko hayo Meneja wa Barabara za Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Mohamed Kuganda alisema kutakuwa na askari wa usalama barabarani katika maeneo hayo ili kuwaongoza watumiaji.
Kuganda alisema lengo la mabadiliko hayo ni kupunguza msongamano wa magari na kuwaandaa wananchi katika mabadiliko mengine madogo yatakayofuata baadaye mradi wa BRT utakapoanza kazi rasmi.
Mhandisi huyo alisema baada ya kukamilika kwa mradi wa mabasi yaendayo haraka, daladala zote zinazotumia Barabara ya Morogoro hazitaruhusiwa kufika katikati ya jiji, badala yake mabasi yaendayo haraka yatafanya kazi hiyo.
Mabasi yatumiayo barabara za Kilwa na Ali Hassan Mwinyi yataendelea kufika katikati ya jiji hata baada ya mradi wa BRT kukakamilika kwa sababu barabara hizo hazina mabasi yaendayo haraka.
“Pia, daladala zote zinazotoka Mnazi Mmoja kwenda Posta, hazitaruhusiwa tena kufika Posta Mpya, badala yake zitatumia Barabara ya Uhuru na kuishia kituo cha Stesheni na kurudi kupitia Barabara ya Samora,” alisema.
Meneja wa Malalamiko ya Waathirika wa Mabadiliko wa Wakala wa Usafiri wa Haraka (Dart), Deus Mutasingwa alisema Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), unashirikiana kwa karibu na wadau wengine kama Sumatra, Manispaa ya Ilala, trafiki na Wizara ya Ujenzi katika kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika kwa ufanisi.
Mutasingwa alisema wanatarajia kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kwa sababu jambo hilo ni geni na litaonekana kuleta usumbufu.
Aliwataka watumiaji wote wa barabara kuwa makini katika kufuata alama za barabarani au mwongozo utakaotolewa.
Mabadiliko yaliyofanyika, pia yanahusisha mabasi yote yanayopita Barabara ya Kilwa ambayo yataishia Stesheni na kurudi kupitia njia hiyohiyo.
Mabasi yanayopita Barabara ya Nyerere na Uhuru yataishia Kituo cha Mnazi Mmoja na kurudi kupitia njia zao. Pia kutakuwa na mabasi yatakayoanzia Mnazi Mmoja kupitia Bibi Titi, Maktaba hadi Posta ya Zamani - Benki ya NBC na kurudi kupitia njia hiyohiyo. Mabasi yote yanayopita Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kwenda katikati ya jiji yataishia katika Kituo cha YMCA Barabara ya Upanga na kurudi kupitia njia hiyo.
KUTOKA MWANANCHI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni