visit here again on mukebez.blogspot.com


CHANGE YOUR LIFE

CHANGE YOUR LIFE
Go to Amazon .com and get the copy of this book to make your life better.

Jumatano, 18 Juni 2014

MDEE AWATAKA WAKULIMA KUIPIGA MAWE SERIKALI

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), amewataka wakulima, wafugaji kuipiga mawe Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutenga sh bilioni 50 kwa ajili ya safari za rais huku ikitenga sh bilioni 51 kwa maendeleo ya kilimo.
Akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015, Mdee alisema serikali haina nia ya dhati ya kuutokomeza umasikini, ikiwemo kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi.
Alibainisha kuwa katika bajeti ya mwaka jana, serikali iliahidi asilimia 10 ya bajeti itakwenda kwenye kilimo, lakini ikaishia kutenga asilimia nne, na bajeti ya mwaka 2014/2015 imetenga sh bilioni 51 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya kilimo.
Alisema kiwango hicho kimepishana kidogo na kile kilichotengwa kwa ajili ya safari za Rais Jakaya Kikwete, ambazo zimetengewa sh bilioni 50.
“Wakulima, wafugaji na wavuvi wanapaswa kuipiga mawe Serikali ya CCM, hapa mmetuletea bajeti, lakini ukiangalia kwa kina utaiona haina dhamira ya kuwasaidia wananchi,” alisema.
Mdee, alisema bajeti ya Wizara ya Kilimo kila mara imekuwa ikitengewa fedha, lakini hazifiki kwa walengwa, hivyo mipango mbalimbali imeshindwa kutekelezeka.
Alisema kuwa serikali kupeleka huduma kwa wananchi ni lazima na sio hiyari, hivyo wabunge wa upinzani wanapokosoa utendaji wa serikali hawafanyi jambo baya bali wanatekeleza wajibu wao.
Aliongeza kuwa serikali kila mara imekuwa ikipewa ushauri mbalimbali, lakini inashindwa kutekeleza jambo linalosababisha kukosa mapato yanayotakiwa.
Alisema miaka minne iliyopita upinzani ulipendekeza kodi ya mishahara kwa wafanyakazi ishuke chini ya asilimia 10, lakini serikali ilishindwa kutekeleza jambo hilo hadi hivi sasa ilipoamua kushusha kutoka asilimia 13 hadi 12.
Aliongeza kuwa Kamati ya Bajeti inafanya kazi kwa niaba ya Bunge na imelalamika inatoa mapendekezo serikalini lakini inapuuzwa hali inayoonyesha serikali haina dhamira ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato visivyowaumiza wananchi.
Mkosamali amvaa Chenge
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), aliituhumu Kamati ya Bajeti kuwa inafanya vikao visivyo na tija ilimradi ihalalishe wajumbe wake kupewa sh 500,000 kwa kila kikao.
Alisema anashangazwa na kamati hiyo kuendelea kulalamikia kupuuzwa kwa ushauri wanaoutoa kwa serikali wakati wana uwezo wa kutoa azimio la kukataa bajeti hadi walichokishauri kifanyiwe kazi.
“Jamani tuwe wakweli hapa, sisi tunalalamika tu wakati uwezo wa kubadilisha mambo tunao, tukubaliane hapa kuikataa bajeti hii mpaka serikali itakapoleta bajeti yenye tija kwa taifa.
“Kamati ya mzee Chenge taarifa yao inalalamika kuanzia mwanzo mpaka mwisho halafu inasema inaunga mkono bajeti, hivi kama si unafiki ni nini? Inakaa hivi sasa na mashirika kujadili kuwapunguzia kodi… hii ni rushwa tupu,” alisema.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alisema serikali imeshindwa kutumia ushauri wa kuanzisha kituo cha uvuvi wa samaki katika bahari kuu, ambako samaki wanavuliwa bila kulipiwa ushuru na kampuni kubwa.
“Nyinyi serikali mna tatizo gani kila mwaka tunawapa ushauri na wataalamu wenu wanaandika ripoti zinazoonyesha umuhimu wa kuanzia kituo cha uvuvi katika bahari kuu, huko tunapoteza mapato mengi lakini hamjali, nyinyi akili zenu zinawaza nini?” alihoji.
Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jaffo (CCM), alisema kiwango cha asilimia kilichopunguzwa kutoka katika kodi inayotozwa kwenye mishahara ni kidogo na hakina msaada kwa wafanyakazi.
Alisema serikali inapaswa kujikita zaidi kwenye kutafuta vyanzo vipya vya mapato badala ya kila kukicha kuwabana wafanyakazi na wananchi.
TANZANIA DAIMA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni