Dar es Salaam. Wakati maelfu ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wakilia na kumboleza kutokana na mvua zilizonyesha kwa siku tatu mfululizo, kwa wengine hali hiyo ilikuwa neema.
Hivi sasa, wakati wenzao wakitathmini hasara na kumalizia misiba kwa walioondokewa na ndugu au jamaa, wao wanahesabu faida na pengine kuombea hali kama hiyo irejee tena ili waendelee kupata kunufaika.
Siku tatu za mwisho wa wiki iliyopita, Jiji la Dar es Salaam lilikumbwa na taharuki iliyotokana na mafuriko. Hata wale wasioishi mabondeni waliiona adha ya mvua hiyo kutokana na maji kutanda karibu kila kona ya jiji.
Kuvusha watu kwenye maji
Hili halikuepukika katika siku hizo za mvua mfululizo kwani kuna baadhi ya maeneo ambayo hakukuwa na usafiri mwingine unaoweza kukuvusha zaidi ya watu hawa.
Kubebwa buku (yaani Sh1,000), kushikwa mkono jero (yaani Sh500). Kauli hiyo ilikuwa ikirudiwa mara kadhaa na vijana waliokuwapo katika eneo la Mto Yombo, karibu na Shule ya Msingi Kilakala Temeke, Dar es Salaam.
“Kuvusha gari tunachaji Sh500, watu wanachajiwa kwa bei tofauti. Ukibebwa unalipa Sh1,000 lakini ukiongozwa kwa kushikwa mkono ni Sh500,” anasema mmoja wa vijana hao aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Pandu. Akizungumzia kuhusu tija ya biashara hiyo, Pandu anasema kuwa ni ya muda mfupi lakini ina faida kwa kuwa hauhitaji kuwa na mtaji wa pesa ama vifaa.
Waendesha bodaboda, bajaji
Kutokana na kuharibika kwa miuondombinu na maji kujaa kwenye barabara uliosababishwa na mvua hizo, usafiri wa daladala uliozoeleka kwa wengi ulikuwa mgumu sana na badala yake pikipiki za abiria, maarufu kama bodaboda, na za matairi matatu (bajaji) zikachukua nafasi.
Kwa kawaida nauli ya bodaboda kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo mpaka Temeke ni Sh 8,000 au Sh10,000, lakini kwa siku hizo tatu nauli ilipanda hadi kufikia Sh30,000.
Mmoja wa waendesha bodaboda wa Tabata Relini, Hussein Ramadhani alisema kuanzia Ijumaa mvua zilipoanza kunyesha pato lake la siku liliongezeka mara mbili.
Dereva huyo aliongeza kuwa mvua hizo zimekuwa baraka kwake na kama zingeendelea kunyesha, angeneemeka maradufu.
HABARI KWA HISANI YA GAAZETI LALEO LA MWANANCHI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni