CCM yawatangazia vita UKAWA
*.Yaagiza Green Guards kupambana nao
22/04/2014|Posted by Danson Kaijage| Kitaifa tangulizi| 0 comments|80 views
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umetangaza vita kwa vyama vya siasa, hususan kwa wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
UVCCM imesisitiza kupambana na wajumbe wa UKAWA watakaotumia mikutano yao ya hadhara kuwakashifu waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.
Vita hiyo ilitangazwa jana na Katibu Mkuu wa UVCCM, Paul Makonda, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa UKAWA kuendelea na maandalizi ya mikutano yao nje ya Bunge.
Mbali ya kuagiza UVCCM ichukue sheria mkononi, Makonda alivitaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua za kisheria wanasiasa aliodai wanasababisha uvunjifu wa amani nchini.
Makonda alisema iwapo vyombo vya dola havitawachukulia hatua watu hao, UVCCM hawatakubali kuona Mwalimu Nyerere, mzee Abeid Aman Karume na Rashid Kawawa wakitukanwa na kudhalilishwa hadharani.
“Hatutakubali tena na ninaomba vijana wote wa ‘Green Guards’ wakae tayari popote watakapoona waasisi wanatukanwa, wachukue hatua. Huu unyonge sasa basi.
“Sisi kama Umoja wa Vijana tunajisikia vibaya sana tunapoona waasisi wa taifa letu wanadhalilishwa na kutukanwa kwa kigezo tu cha kujenga hoja na kutafuta kuaminika na kukubalika.
“Nimejaribu kupitia kanuni zetu, kanuni ya 46 (e) ya Bunge Maalumu inasema ni marufuku au hairuhusiwi kutumia jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar au marais wastaafu, kuwatumia kwa dhihaka au kwa kutaka kushawishi hoja fulani iweze kukubalika, na hizi kanuni zimepitishwa na wajumbe wote lakini kwa masikitiko makubwa, Mwalimu Nyerere ameonekana ni aliyezoea vya kunyonga, kwa sababu nimeipitia ile ‘Hansard’ kwa umakini zaidi kuona maneno ambayo alikuwa anatumia Mheshimiwa Tundu Lissu, ni maneno ya kufedhehesha na wala si maneno yanayostahili kwa viongozi ambao wanaheshimika,” alisema.
Akizungumzia kuhusu wapinzani kutoka ndani ya Bunge, alisema watu wenye hoja hawakimbii bali hupambana kwa hoja.
“Leo hii mnalisusa Bunge mnaenda kwa wananchi, mnaenda kuwaambia nini? Hapa kinachotafutwa ni nchi yetu isitawalike,” alisema.
Hata hivyo Makonda katika taarifa hiyo amepotosha umma kwani Lissu hajawahi kumkashifu wala kumtukana Mwalimu Nyerere wala mzee Karume.
Wakati akitoa maoni ya watu wachache bungeni, Lissu alisema Mwalimu Nyerere ndiye aliyeiua Tanganyika wakati hakuwa na mamlaka kisheria kufanya hivyo.
Sehemu ya hotuba ya Lissu iliyokaririwa na gazeti hili
Lissu alisema wajumbe wengi wamekuwa wakipotosha umma kwamba kukubali serikali tatu ni kuvunja hati ya makubaliano ya muungano ambayo haipo wala haijawahi kutolewa mbele ya hadhara.
“Swali la msingi linalohitaji kuulizwa, je, hati hii ipo, swali la pili je, hati hii ni halali? Swali la tatu, kama hati hii ipo na ni halali je, muungano huu ni halali?,” alihoji.
Lissu alisema hakuna ushahidi kwamba kuna hati ya muungano kwa kuwa hata Umoja wa Mataifa kunakoelezwa ilipelekwa wamethibitisha hakuna jambo hilo.
“Hati ya Muungano haipo Zanzibar wala Tanganyika, haipo UN wala bungeni, sasa hiki kilichozungumzwa na wengi kuwa kuanzisha muundo wa serikali tatu ni kuvunja hati hizo ni uongo tu, zama za uongo sasa zimefikia mwisho.
“Nusu karne ya uongo sasa ikome, tuambiane ukweli hivi sasa, waliozoea vya kunyonga kamwe hawawezi vya kuchinja, mimi nawataka wajumbe wenzangu tufikie mwisho wa kudanganya,” alisema.
“Ni nani aliyeshuhudia wakati wa kutiliana saini makubaliano ya muungano? Hakuna walioshuhudia, wale wote walioshuhudia jambo hilo waliuawa, sasa mnahofia nini kuingia kwenye serikali tatu?” alihoji.
Bunge la Tanganyika lilithibitisha kuungana na Zanzibar lakini Zanzibar haikuridhia jambo hilo kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali zilizopo.
Lissu alisema nyaraka zinaonyesha kuwa Aprili 4, mwaka 1964 siku moja baada ya muungano Mwanasheria Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Constantine Paulo, aliandika barua kwa ubalozi wa Tanganyika akiwaambia wamesikia kuwa wameungana na Zanzibar, wapeleke hati ya makubaliano hayo ili iweze kupata usajili wa Umoja wa Mataifa itambulike kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Alisema Mei 6, mwaka huo huo siku kumi baadaye Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanganyika ikapeleka tamko rasmi kwamba kweli wameungana na hati ya muungano, wameiambatanisha na ‘noticefication.’
Aliongeza kuwa Mei 14, wiki moja baadaye mwanasheria huyo akaandika ‘telex’ kwa serikali Tanzania akiwataka Watanzania wawatumie nakala mbili za hati ya makubalino ya muungano ili waisajili kwa mujibu wa ibara ya 102 ya United Nations Charter.
“Taarifa hii inaamanisha kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania iliposema kwamba tumewaleteeni hawakupeleka, sasa mwenyekiti ushahidi kwamba Umoja wa Mataifa haujawahi kupelekewa hati ya muungano umepatikana Machi 3, 2009 wakati ofisa habari za kisheria wa kitengo cha mikataba ya kitaifa wa Umoja wa Mataifa, ofisi inayoshughulikia masuala ya kisheria alipomwandikia mtafiti mmoja aliyeandika kitabu kwamba hakuna ushahidi wowote kwamba hati ya muungano ilisajiliwa kwenye sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.
“Kama ingesajiliwa kungekuwa na hati ya usajili iliyoambatanishwa, nimeangalia hakuna kitu kama hicho, Mwenyekiti, hati ya makubaliano ya muungano haipo Umoja wa Mataifa na haipo Tanzania na kuna ushahidi kwamba haipo Tanzania,” alisema.
Alisema mwaka 2005 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilishitakiwa Mahakama Kuu ya Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Idd Pandu Hassan, aliambiwa apeleke hati ya makubaliano ya muungano yenye saini ya Nyerere na Karume.
“Maneno ya Mwanasheia Mkuu wa Zanzibar yanasema hivi kwa barua yake ya tarehe 22/6/2005, anasema; ‘ofisi yangu haikuweka kumbukumbu ya mkataba wa asili (original) wa muungano wa Tangayika na Zanzibar tarehe 26/4/19964’” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni