Friday, April 18, 2014
TAARIFA KUTOKA TFF LEO Aprili 18, 2014
PAZIA VPL LAFUNGWA, AZAM KUKABIDHIWA KOMBE CHAMAZI
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inafikia tamati kesho (Aprili 19 mwaka huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani, huku mabingwa wapya Azam wakikabidhiwa kombe lao Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mechi yao dhidi ya JKT Ruvu.
Mechi zote saba zitachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni ambapo Yanga na Simba zitakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mechi ambayo viingilio vyake ni sh. 5,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
Tayari tiketi zimeanza kuuzwa leo (Aprili 18 mwaka huu) katika vituo saba vya; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kariakoo (Kidongo Chekundu), Buguruni Shell, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, Ubungo OilCom, Dar Live Mbagala na Uwanja wa Taifa.
Mechi nyingine zitakuwa kati ya Tanzania Prisons na Ashanti United (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Rhino Rangers na Ruvu Shooting (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City na Mgambo Shooting (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Oljoro JKT na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha) na Coastal Union na Kagera Sugar (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga).
MICHUANO YA BEACH SOCCER KUANZA JUMAPILI
Michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (Beach Soccer) inazinduliwa rasmi keshokutwa (Aprili 20 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni, Dar es Salaam na kushirikisha timu 13.
Uzinduzi huo utaanza saa 5 asubuhi na mechi zitachezwa hadi saa 11 jioni. Michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini inashirikisha timu 13 kutoka vyuo mbalimbali vya jijini Dar es Salaam.
Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Ardhi (AU), Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Michuano hiyo itakuwa inachezwa Jumamosi na Jumapili kwenye fukwe za Escape One na Gorilla Beach iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.
WAZOEFU TAIFA STARS KUTAJWA KESHO
Wachezaji wazoefu wa Taifa Stars watakaoungana na wale 16 waliopatikana katika mpango wa maboresho wa timu hiyo watatangazwa kesho (Aprili 19 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itapiga kambi kwenye hoteli ya Kunduchi Beach kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi itakayochezwa Aprili 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji waliopatikana katika mpango wa maboresho ya Stars wanatarajiwa kuwasili leo (Aprili 18 mwaka huu), na kwenda moja kwa moja kambini kuwasubiri wenzao watakaotajwa kesho (Aprili 19 mwaka huu).
Wachezaji hao ni kipa Benedicto Tinoko Simwanda (Mara), Emma Namwondo Simwanda (Temeke), Joram Nason Mgeveje (Iringa), Omari Ally Kindamba (Temeke), Edward Peter Mayunga (Kaskazini Pemba), Shiraz Abdallah Sozigwa (Ilala), Yusuf Suleiman Mlipili (Temeke) na Said Juma Ally (Mjini Magharibi).
Wengine ni Abubakar Ally Mohamed (Kusini Unguja), Hashim Ramadhan Magona (Shinyanga), Omari Athumani Nyenje (Mtwara), Chunga Said Zito (Manyara), Mohammed Seif Saidi (Kusini Pemba),Ayoub Kasim Lipati (Ilala), Abdurahman Othman Ally (Mjini Magharibi) na Paul Michael Bundara (Ilala).
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Friday, April 18, 2014
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni