ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo, amekemea tabia ya utoaji mimba inayofanywa na baadhi ya wanawake nchini kwani kufanya hivyo ni kupingana na amri ya Mungu.
Pia amekemea dhana potofu ya ndoa za jinsia moja kwa kisingizio cha kukataa kupata watoto.
Akizungumza jana wakati wa misa iliyowakutanisha wanakwaya wote wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Pengo alisema kuwa baadhi ya wanawake hivi sasa wana mawazo kwamba mtoto mmoja anatosha.
Alisema kina mama wenye mawazo hayo wanapopata mimba nyingine, huamua kuzitoa jambo ambalo si sahihi na haikubaliki mbele ya Mungu.
Alisema wakati kina mama wengine wakiwa na mawazo na mtoto mmoja, wapo wanaokataa kuwa na watoto, hivyo kuamua kuingia kwenye ndoa za jinsia moja.
“Dhana potofu kwamba mtoto mmoja anatosha, kufikiria kwamba unaweza kuwa na familia bila watoto au unapata mimba halafu unaambiwa nenda kwa mtaalamu atoe, hapo unashindwa kusimama kama mama au dada katika imani yako, kwa kufanya hivyo mnakwenda kinyume cha amri ya Mungu inavyotaka,” alisema.
Pengo alisema familia nyingi zina changamoto nyingi kama kutoheshimu uhai wa mtu, kutomwamini Mungu na hata kupotosha maana halisi ya familia yenyewe kwa kufanya mambo kinyume cha sheria za kanisa.
Hata hivyo Pengo alisema, mwanamke ana umuhimu mkubwa katika familia, tena anaweza kuwa chanzo cha mabadiliko kama wasipopotoshwa na wasipofikiria mawazo mabaya ambayo yatahatarisha amani na upendo katika taifa.
“Mtu anayeweza kuwa chanzo cha mabadiliko katika familia ni mwanamke, kinachotakiwa hapa, hawa kina mama wasipotoshwe na wasifikirie mawazo mabaya,” alisema,
Aidha, alisema mambo mengi yanayofanywa na wanawake ni mazuri lakini huchukua muda mrefu kutambulika katika jamii hivyo kurudisha nyuma kasi ya maendeleo.
KUTOKA MTANZANIA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni