HAMAD NURUABEID: Mtoto wa miaka 4 anayelisha familia
ANA miaka minne, anakula mlo mmoja saa 9 alasiri, mlo huo ukipatikana huanza kufanya kazi ya kuokota chupa za maji.
Ikiwa ni zaidi ya miaka 10 imepita tangu mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto ulipotiwa saini, bado jamii kadhaa zinashindwa kutekeleza haki hizo, na hivyo kuwafanya watoto kuwa na maisha magumu.
Na ni ukweli ulio wazi kwamba mafanikio ya mtu mzima yanachangiwa na malezi ya utotoni pamoja na mazingira na mwingiliano wa mazingira na jamii yake.
Kama wazazi au walezi wakifanya jitihada kumjenga mtoto na kumwandaa kuwa mtu makini anayejitambua, ni dhahiri mchango wake kwa jamii utakuwa mkubwa.
Makala hii inamuangazia Hamad Nuruabeid (4) wa Kata ya Mkata Mashariki, Wilaya ya Handeni, Tanga anayeokota chupa za maji na kuziuza lengo likiwa ni kuwezesha familia yake kupata chakula.
Nilikuwa katika safari ya kikazi Kata ya Mkata. Nilifika usiku na kulala katika nyumba ya wageni iitwayo Esperanto. Kulipokucha nilikaa katika eneo hilo kwa lengo la kujipatia kifungua kinywa, ndipo alipopita Hamad akiwa na mfuko wenye chupa za maji na kuokota chupa iliyokuwa meza ya jirani na nilipokaa.
Nilimtazama na kushawishika kumuita na kumuuliza kwanini yupo eneo hilo muda huo na chupa hizo anazipeleka wapi?
Baada ya kumuita, alikuja na kunisalimia. Nikavuta kiti na kumwambia aketi, nikamuomba mhudumu ampatie chai. Uso wake ukaonyesha furaha.
Alikunywa chai kwa furaha, akasema asante. Nikamwambia nataka kuongea nae, na kwa sauti ndogo akasema; “mama atanichapa akitoka shamba.”
Nilimsihi na akakubali baada ya kumwambia kuwa nitaenda kwa mama yake kuzungumza nae pia. Kilichonistaajabisha, Hamad ni mtoto mwenye upeo mkubwa wa utambuzi wa mambo, hasa unapomuuliza maswali.
Hamad ana historia isiyo nzuri katika miaka minne aliyonayo sasa. Wamezaliwa wawili akiwa na dada yake aitwaye Rehema anayesoma darasa la kwanza huku akienda shule kwa kusuasua.
Mtoto huyu mwenye upeo wa hali ya juu, aliweza kunieleza masahibu anayokutana nayo katika kazi yake ya kuokota chupa za maji.
Anasema: “Huwa naamka asubuhi, mama na baba wakiwa wanaenda shamba, mimi naenda kuokota chupa, natembea jalalani, barabarani na kama hapa (Esperanto), naokota zikijaa nazipeleka nyumbani na mama akirudi shamba anaziuza.”
Hamad anatembea akiwa hana viatu hali iliyosababisha kuwa na kidonda kisichopona katika mguu wake.
Anasema kuwa kuna vitu vingi anavitamani, lakini mara zote anapomwambia mama yake amnunulie amekuwa hatimizi.
Mtoto huyu ana nguo moja iliyochafuka sana, anapita sehemu hatarishi, anasema kuwa anatamani kwenda shule, lakini hajapelekwa kwa sababu mama yake humwambia bado mdogo.
Nyumba anayoishi Hamad inasikitisha, kwani imeharibika na ukiingia ndani unamuona hata aliye nje, hana mahali pazuri pa kulala yeye pamoja na dada yake.
Huzuni ya Hamad ni akiona wenzake wanakula chakula kizuri, wanavaa vizuri wakiwa na viatu, wakati yeye hana na ana nguo moja aliyoivaa pekee.
Mama wa mtoto huyu aliyejitambulisha kwa jina la Mama Rehema, anasema kuwa ugumu wa maisha ndio unafanya Hamad aokote chupa.
Anasema kuwa yeye hana namna ya kufanya kutokana na baba wa mtoto huyo nae kutokuwa na uwezo.
“Kuliko kukaa nyumbani, ni afadhali aokote chupa, dada yake akirudi shule nae anaenda kuokota chupa, maisha ni magumu, hasa hapa Mkata, najitahidi wale hiyo saa tisa ili chakula kikae tumboni muda mwingi, ila wameshazoea kula muda huo, hawana shida wanangu.
“Asubuhi tunaamka na kuelekea shamba, hasa ikiwa kipindi cha kulima. Lakini wakati mwingine mimi nakuwa nauza mboga au naokota chupa zilizokwisha maji ili tunachokusanya kitusaidie kwa chakula, tatizo tu wanaonunua chupa hizo, hununua kwa hela ndogo baada ya kuwapelekea, matokeo yake sisi tunaendelea kuwa na maisha magumu kila siku,” anasema Mama Rehema.
Mama huyo aliyekata tamaa, anasema amekuwa akitamani kuwafanya watoto wake wawe na maisha mazuri, hata ya kula mara tatu kwa siku, lakini anashindwa kutokana na kukosa uwezo.
Anaeleza: “Hamad ana uwezo wa kuokota hadi kilo kumi za chupa kama siku hiyo chupa zinakuwa nyingi. Lakini zikiwa chache anakusanya kilo nne au sita… Tumempa mfuko na anapookota na kujaa analeta nyumbani na tunaenda kuziuza kilo moja kwa sh 500 au 450, basi tunapata hela ya chakula, lakini wakati mwingine anaokota chupa chache.”
Umoja wa Mataifa (UN) umetoa azimio juu ya haki za watoto (Convention on the Rights of the Child) lililokubaliwa na karibu nchi zote za dunia isipokuwa Marekani na Somalia kuwa mkataba wa kimataifa, likieleza kwamba utoto ni kipindi hadi kufikia umri wa miaka 18.
Mkataba wa Kiafrika juu ya haki na ustawi wa watoto (African Charter on the Rights and Welfare of the Child) uliokubaliwa na Umoja wa Afrika unamwona pia mtoto ni kutoka anapozaliwa hadi anapofikia umri wa miaka 18. Haki hizi Hamad hazifahamu, hazijamsaidia.
Hamad anahuzunisha sana hasa kwa umri alionao na kazi anazozifanya, huku akitembea umbali mrefu bila kula na akipita sehemu zenye hatari.
Mtoto huyu anapenda kusoma, lakini hajaanza hata chekechea, anapenda avae vizuri, lakini wazazi hawana uwezo.
Kuna watoto wengine wana mavazi hadi wanayavuruga, kwanini kama mzazi usijitoe kwa mtoto huyu kwa kumpatia msaada wa mavazi, fedha na hata chakula?
Hamad ana wazazi wote, lakini hawana uwezo, tuungane mimi na wewe katika kukomboa watoto wasio na uwezo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni