KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lazaro, ameendelea kujikanyaga kuhusu sakata la kukodisha ndege chakavu aina ya Bombardier CRJ 200 na kutangaza kwamba wameinunua nchini Canada.
WakatiTanzania Daimailipofichua ukweli kwamba ndege hiyo haijanunuliwa kama ATCL ilivyoripoti na badala yake imekodishwa katika Shirika la Ndege la Fly 540 la nchini Kenya ambalo limetetereka kiuchumi, ilikana taarifa hizo kwa kusema hazina ukweli.
Baada ya kuendelea kuandika ukweli wa jambo hilo, ATCL ilikiri katika taarifa yake kwamba ndege hiyo imekodiwa, lakini wakishindwa kuweka bayana mahali ilikokodiwa na gharama yake katika kipindi hicho cha wiki tisa.
Tanzania Daimailipomtafuta Kapteni Lazaro ili aelezee ukweli, aliishia kutoa lawama kwa wanahabari walioweka wazi sakata hilo.
“Wewe si ndiyo umekuwa ukiandika ‘articles’ ukitudhalilisha, hivyo unataka niweke wazi kitu gani? Mnataka niwasaidie nini? Na pia nataka kujua chuki yenu ni ATCL au mtu binafsi?
“Mmekuwa mkinichokoza pindi ninapokuwa kwenye mikutano, kwanza naomba mnifafanulie chuki yenu ni mimi binafsi au chuki yenu ni kampuni? Kama ni mimi au kampuni nambieni. Si mmedhamiria kuendelea kuandika endeleeni. Kumbuka mmekuwa mkiandika na mmetukana sana, sasa ukinipigia kutaka ufafanuzi nitawafafanulia nini wakati mmeshaandika na kutukana? Mmedhalilisha kampuni na watu hivyo mimi nitawasaidia nini?” alihoji.
Lazaro ametoa malalamiko hayo baada ya gazeti hili kuandika kwamba ndege aina ya Bombardier CRJ 200 ni mzigo kwa taifa kutokana na ukweli kwamba imeshatumika Kenya.
Uchunguzi huo ulibaini ndege hiyo imekuwa ikitumia dola 4,500 (sh milioni 7.2) kwa saa pindi inapokuwa angani na inapotua kiwanjani hugharimu dola 200 (sh 320,000).
Ndege hiyo iliyokodiwa kwa muda wa wiki tisa, imekuwa ikiigharimu ATCL kuwalipia marubani wake watano kutoka Kenya malipo ya dola 500 (sh 800,000) kwa siku kwa ajili ya malazi ya hoteli ya hadhi ya nyota tano.
Gharama nyingine za marubani hao ni usafiri inayofikia kiasi cha dola 200 (sh milioni 1.6) kwa wote watano.
Tanzania Daima liligundua kwamba baada ya kukodiwa kwa ndege hiyo, gharama zake za kuitoa Kenya na kufika nchini zilikuwa dola 6,000 (sh milioni 9.6) na pindi itakapomaliza muda wake wa wiki tisa itatakiwa kurudishwa kwa kiasi hicho hicho cha fedha.
Vyanzo vyetu kutoka ndani ya ATCL vilieleza kuwa kama shirika hilo lingekuwa na nia ya kupunguza gharama ya uendeshaji bora lingenunua ndege aina ya DASH-8 inayotumiwa na shirika hilo ikiwa na uwezo wa kubeba watu 50 kama ilivyo kwa CRJ 200.
Ndege aina ya DASH-8 pamoja na kufanya kazi sawa na CRJ 200, lakini gharama zake za uendeshaji zimekuwa nafuu kwa sababu marubani, wahandisi wake wanatokea nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni