Dar es Salaam.Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania, (Chawata), Shida Salum, yuko katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Ami, Masaki, Dar es Salaam akisumbuliwa na maradhi ya saratani.
Shida ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na mama mzazi wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amelazwa tangu juzi. Alianza kusumbuliwa na maradhi hayo mapema Agosti mwaka jana lakini hali yake ilibadilika mapema mwaka huu akiwa mjini Dodoma akisubiri kuapishwa pamoja na wajumbe wengine wa Bunge Maalumu la Katiba.
Akizungumza hospitalini hapo jana, Zitto alisema baada ya hali ya mama yake kuwa mbaya alishindwa kuendelea kukaa Dodoma kusubiri kuapishwa na alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambako aligundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi na kupatiwa tiba kwa mwezi mmoja kabla ya kupelekwa India kwa matibabu zaidi.
Alisema kabla ya kupelekwa hospitalini hapo, alikuwa akiendelea kupata matibabu akiwa nyumbani, lakini hali yake ilibadilika juzi.
Zitto alisema hali ya mama yake haijatengemaa tangu aanze kusumbuliwa na maradhi hayo. Alisema kutokana na maradhi hayo ya mama yake, ameshindwa kuhudhuria Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.
“Hali ya mama kwa kweli siyo nzuri, lakini nina imani itakuwa nzuri na kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa kama zamani,” alisema Kabwe.
Tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti, Zitto alionekana Dodoma mara moja tu, siku ilipowasilishwa Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni