Morogoro. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia Mohamed Mgende (59) mlinzi na mkazi wa Msamvu Ndege Wengi kwa tuhuma za kumbaka binti wa miaka 12, mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Msamvu B.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard Paulo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 21, mwaka huu saa 11 jioni, Manispaa ya Morogoro.
Kamanda Paulo alisema kuwa, mtuhumiwa alikutwa chumbani akiwa na binti huyo na inaaminika alikuwa akijiandaa kumbaka kwa vile alishavua nguo na kujifunga taulo.
Akielezea namna taarifa hizo zilivyowafikia, Paulo alisema binti huyo alimweleza mwalimu wake (jina linahifadhiwa) kuhusu namna anavyofanyiwa vitendo vya ubakaji na mtuhumiwa huyo na ndipo mwalimu huyo alipotoa taarifa polisi.
Alisema mwanafunzi huyo alimweleza mwalimu wake kuwa, alianza kubakwa na mtuhumiwa huyo tangu akiwa darasa la nne na kwamba alishindwa kuwaeleza wazazi wake kwa sababu mtuhumiwa alimtishia kumuua kama angesema.
“Taarifa za awali zinaonyesha kuwa mtuhumiwa alikuwa akiishi jirani na familia anayotoka binti huyo na kila alipombaka alimnunulia chips na kumpa Sh200 au 500,” alisema Kamanda Paul.
Pia mtuhumiwa huyo alikuwa akimdanganya binti huyo kuwa anamiliki ghorofa jambo ambalo siyo kweli kwani ghorofa alilomwonyesha alikuwa akifanya kazi kama mlinzi.
“Kuna taarifa zaidi kuwa alikuwa akiwabaka mabinti wengine, hatuwezi kuthibitisha kwa sasa ila tunaendelea na uchunguzi,” alisema.
Aliwataka wananchi kushirikiana na polisi ili kubaini kama alishawahi kuwafanyia vitendo hivyo watoto wengine.
Mama mzazi wa binti huyo (jina limehifadhiwa) alipata mshtuko na kupoteza fahamu.
VIA:MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni