TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, jana ilivuna ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Malawi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo ni ishara njema kwa Stars inayosaka makali ya kuwanyoa Zimbabwe na kuwatupa nje ya kampeni ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwakani nchini Morocco.
Stars inakabiliwa na mechi hiyo ya marudiano hatua ya kwanza ya kampeni za kwenda Morocco dhidi ya Zimbabwe itakayochezwa Juni Mosi, mjini Harare kuwania tiketi ya kutinga hatua ya pili.
Kama Stars itafanikiwa kuing’oa Zimbabwe, itakutana na mshindi wa jumla kati ya Msumbiji na Sudan Kusini, na ikivuka hapo itaungana na timu za Zambia, Cape Verde na Niger katika kundi F.
Mechi ya jana ilianza kwa kasi ndogo, huku kila timu ikijitahidi kumsoma mwenzie ili kuepuka sare ya bila kufungana kama ilivyokuwa mechi ya kwanza ya kirafiki baina ya nchi hizo iliyochezwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya mapema mwezi huu.
Dakika ya 17, Stars nusura ijipatie bao, lakini shuti la umbali wa mita 20 la Kelvin Friday lilipaa sentimita chache juu ya lango la Malawi.
Dakika ya 37, mshambuliaji Amri Kiemba aliipatia Stars bao pekee kwa shuti dogo, akimalizia pasi ya kiungo-mkabaji Shomari Kapombe aliyepanda kusaidia mashambulizi.
Kipa wa Stars, Deogratius Munishi ‘Dida’ alifanya kazi ya ziada na kukataa katakata nyavu zake zisitikiswe, baada ya kupangua shuti maridadi la Chimango Kaira, aliyefumua mkwaju huo kutokea upande wa kushoto kwenda lango la Kaskazini.
Hadi filimbi ya mwamuzi Israel Nkongo kuashiria mapumziko, Stars ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili, kilianza kwa Malawi kushambulia wakisaka bao la kusawazisha na wakakosa mabao matatu dakika za 47, 61 na 85 kwa mtokea benchi Rodrick Gonani kukosa baada ya kipa wa Stars, Dida kupangua na kuwa kona tasa.
Gonani alikosa bao jingine kwa staili hiyo akiunga pasi ya Bashiri Maunde katika lango tupu, Dida akiwa amepotea.
Stars inasafiri kwenda Zimbabwe kusaka sare, huku wenyeji wakitakiwa kushinda zaidi ya mabao 2-0 ili kusonga mbele.
Mara ya kwanza na mwisho kwa Stars kucheza fainali za Afrika ni mwaka 1980, hivyo mkakati wa timu hiyo ni kucheza fainali hizo kwa mara ya pili hapo mwakani.
Stars: Deogratius Munishi ‘Dida,’ Himid Mao/Haruna Chanongo, Edward Charles, Said Moradi, Joram Mgezeke, Shomari Kapombe, Simon Msuva/Ramadhani Singano, Erasto Nyoni, Kelvin Friday/Amri Kiemba/Mwinyi Kazimoto na Khamisi Mcha.
Malawi: Richard Chipuwa, Moses Chabvula, Limbikani Mzava/Christopher Banda, John Lanjesi, Foster Namwera, Phillipe Masiye Young Chimodzi/Bashiri Maunde, Gabadinho Mhango/Rodrick Gonani, Chimango Kaira, Joseph Kamwendo na Atusaghe Nyondo/Robin Ngalande.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni