SINA hakika kama watu wote duniani wana kawaida ya kurithi mali za wazazi wao pindi wanapofariki, lakini nina uhakika utamaduni huu upo kwa sehemu kubwa sana katika jamii zetu sisi Waafrika na hususan Watanzania, ingawa kuna tofauti kadha wa kadha za jinsi ya kugawa au kugawana.
Pamoja na kutambua kuwa utamaduni huu upo miongoni mwetu, lakini pia sina hakika kama kweli Watanzania wote tunafahamu vema sheria zinazotuongoza katika migawanyo ya mali pale inapotokea mzazi amefariki na wanafamilia wakaamua kugawana bila ya kuzingatia wosia wa marehemu.
Katika hali ya kawaida ya maisha yetu sisi wanadamu, ni dhahiri kitaaluma watu wote haiwezekani tukawa wanasheria, lakini kwa uwepo wa hao wanataaluma ya sheria, na sisi wengine pale linapotokea jambo fulani linalohitaji utatuzi wa kisheria basi ni vema kuwatafuta ili watupe miongozo ya jinsi ya kutatua mambo yetu.
Tusipowatafuta watu wenye taaluma hiyo tunaweza kujikuta tunaingia kwenye matatizo makubwa zaidi ya hayo tuliyokuwa tunakusudia kuyatatua.
Nasema hivi kutokana na wanafamilia fulani jijini Dar es Salaam ambao mbali ya kuwa na watu kadhaa waliobahatika kwenda shule vizuri, cha ajabu mara baada ya baba yao kufariki watoto wote wa marehemu pamoja na baadhi ya ndugu zao wengine wakajikuta wanaingia katika mzozo mkubwa uliosababisha hadi kutishiana maisha, kisa? Jinsi ya kugawana mali alizoziacha baba yao.
Mzee huyo ambaye katika maisha yake alioa mara tatu ambapo aliwataliki wake wawili (wa kwanza na wa pili) kabla ya mauti kumkuta, lakini alitambua kuwa wanawake alioishinao pamoja na watoto wao wote wana haki ya mgawo wa mali zake.
Kwa busara zake aliamua kuandika kabisa mgawanyo kamili wa mali zake ili kuepusha shari ambayo alitegemea ingeweza kutokea kama asingeandika urithi na kuukabidhi kwa mwanasheria.
Baada ya mauti kumfika mzee huyo, mmoja wa wana ndugu aliwasomea wosia aliouacha juu ya mgawanyo wa mali zake, ambao ulifanana kidogo na ule wa Mzee Madiba kwa kuwapa wanafamilia wote pamoja na baadhi ya ndugu zake wa karibu, lakini akamtema kabisa katika orodha ya mgawo huo mmoja wa wake zake kama alivyofanyiwa Winnie Mandela!
Katika hali ya kushangaza tofauti na matarajio ya wengi kuwa mara baada ya wosia wa marehemu kusomwa, tena ukiwa umetoka kwa mwanasheria ungerahisisha zoezi zima la mgawanyo wa mali za marehemu, lakini kwa wanafamilia hiyo hali ikawa kinyume kabisa!
Hakuna aliyetaka kukubaliana na wosia huo na kudai kuwa umechakachuliwa na wala hawatambui cha mwanasheria wala huyo ndugu yao – mzee aliyekabidhiwa wosia huo na mwanasheria ili ausome kwa wanafamilia pamoja na watu wote waliokuwepo hapo msibani!
Moja ya kitu ambacho marehemu alisisitiza sana kwa familia yake kupitia wosia huo, ni kuwataka wasithubutu kuiuza nyumba yake bali wanaweza kuipangisha ili pesa za kodi ziwasaidie wadogo zao wadogo ambao bado wapo shuleni.
Kutokana na dalili za wanafamilia hao kuonyesha kutotaka kutambua kuwa kuna mambo ya kuzingatiwa kisheria katika mgawanyo wa urithi tangu pale walipokataa kuukubali wosia wa marehemu baada ya kusomwa, kabla hata mzee wao hajamaliza wiki moja kaburini tangu azikwe, tayari walikwishapata mteja wa kumuuzia nyumba waliyosisitizwa wasiiuze!
Hatimaye wakafanikiwa kumpata mnunuzi na wakaiuza nyumba hiyo kwa milioni kadhaa za nguvu huku nafsi zao zikiwa zimejaa furaha kubwa sana.
Kwa ulimbukeni wao walidhani hizo sh milioni 200 walizofanikiwa kuzipata kwa kuiuza hiyo nyumba wangekaa nazo katika kipindi cha maisha yao yote, wakagawana kwa mbwembe nyingi na kuanza kufanya mambo kibao kwa pupa ikiwa ni pamoja na matanuzi ya jeuri ya pesa.
Sasa pesa imekatika, nyumba ya baba yao haipo tena, wadogo zao shule ni mgogoro mtupu, na wao wenyewe wanaugulia majeraha ya kufulia bila sabuni! Je, leo hii watakuwa wageni wa nani?
Hayo siyo mambo hata kidogo, kwanini mkatae wosia wa baba yenu aliyewaandikia kabla hajafa? Sasa baba hayupo tena duniani, nyumba nayo mmeinywa na nyinyi wenyewe kila siku ni mifarakano.
Msije mkasingizia mmerogwa, hapo hakuna cha mchawi wala mlozi, bali hizo ni dalili za mwanzo wa laana ya kwenda kinyume na matakwa ya marehemu baba yenu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni