visit here again on mukebez.blogspot.com


CHANGE YOUR LIFE

CHANGE YOUR LIFE
Go to Amazon .com and get the copy of this book to make your life better.

Ijumaa, 9 Mei 2014

PUNGUZO LA BEI NI ADUI MKUBWA KWA WAPINZANI WA IPTL.

Hofu ya kupoteza soko kwa makampuni ya kigeni yanayozalisha umeme dhidi ya makampuni ya kitanzania imetajwa kuwa chanzo cha vita dhidi ya kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Chanzo cha uhakika kutoka Wizara ya Nishati na Madini kimetoa taarifa hiyo kwa gazeti hili jana kuwa kwa zaidi ya muongo mmoja, kampuni za kigeni zimekuwa zikipata faida kubwa kwa kuzalisha umeme na kuuza kwa bei ya juu nchini.
Kampuni ya IPTL ambayo inamilikiwa na kampuni ya kizalendo, Pan African Power Solutions Tanzania Limited (PAP) iliishtua dunia mwishoni mwa mwaka jana pale ilipotangaza dhamira yake ya kushusha bei zake kutoka senti za Kimarekani 26 na 30 ya sasa mpaka senti za Kimarekani sita (6) na nane (8) kwa kila unit, pale itakapobadilisha mitambo yake kuweza kutumia gesi badala ya mafuta.
Kwa sasa, makampuni mengine katika soko yanatoza kati ya senti za Kimarekani 38 na 60 kwa kila unit. “Watanzania wasidanganywe na taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa IPTL ilinunuliwa na PAP bila kufuata sheria. Kuna kampeni ya kupakana matope kwa tamaa ya kuzalisha umeme kwa watanzania kutokana na biashara hii kuwa na faida kubwa katika sekta hii muhimu kiuchumi ", chanzo hicho kilisema.
Aidha, kampuni ya PAP katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana, imesema kuwa kampuni imeshtushwa na baadhi ya wawekezaji katika sekta hiyo pamoja na wanasiasa kuanzisha vita dhidi yao mara baada ya kutangaza kupunguza gharama za umeme.
Uongozi wa kampuni hiyo umesema kuwa watanzania watafurahia gharama hizo za chini baada ya utekelezaji wa mkakati wao wa utanuzi na ubadilishaji wa mfumo wa mitambo yao ambao utaongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme kutoka mega wati 100 za sasa mpaka mega wati 500.
Taarifa fupi iliyotolewa jana na katibu na mshauri wa maswala ya sheria wa IPTL/PAP, Bw Joseph Makandege, imesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikikumbana na changamoto ambazo zinajaribu kuzorotesha jitihada za uongozi mpya za kuleta mabadiliko ambayo yatapelekea kampuni hiyo kuanza kuzalisha umeme wenye gharama nafuu kwa watanzania wote.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya machapisho mbalimbali ya vyombo vya habari yanayoishutumu kampuni hiyo kutoa hongo kwa wajumbe wa kamati ya bunge ya nishati na madini kulinda matakwa yao au kuwalinda dhidi ya tuhuma mbali mbali wanazo husishwa nazo.
"Uongozi wa PAP katu haijapendezwa na jitihada za kuiangusha kampuni badala ya kushirikiana katika kuhakikisha kuwa tunazalisha umeme ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa hili na walaji wote nchi nzima.
"Tukiwa kama kampuni ya ufuaji umeme, tunaelewa faida za kiuchumi zitokanazo na umeme wa gharama nafuu kwa mteja mmoja mmoja na kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi nzima. Kwa sababu hiyo ndiyo maana sasa tumeelekeza jitihada zetu katika kuona ni jinsi gani ya kuzaliza umeme wa gharama nafuu ambao utasaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi ya nchi hii, pasipo kuingia katika malumbano ambayo yataturudisha nyuma na kushindwa kutekeleza lengo letu la kuwekeza vilivyo katika sekta hii muhimu," ilisomeka taarifa hiyo.
Bw. Makandege alisema kuwa kampuni yake imeamua kutafuta njia nzuri ya kuzalisha umeme wa gharama nafuu, ukilinganisha na wazalishaji wengine katika soko, sababu inaamini katika kutumia uwepo wake kuboresha maisha ya wateja wake na kuleta mabadiliko katika jamii inayoizunguka.
"Uongozi mpya wa IPTL/PAP unaamini katika kuwapatia wateja wake matokeo yaliyo chanya. Njia pekee ya kulifanya hili ni kutoa bidhaa/huduma zenye gharama nafuu kwa wateja, licha ya wateja hao kuwa na viwango tofauti vya kimapato," alisema.
Mbali na uzalishaji wa umeme, IPTL/PAP imekuwa ikijihusisha na shughuli mbali mbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kuwajengea vijana uwezo wa kifedha ili kuweza kuanzisha Saccos yao ambayo itawasaidia kujijenga kiuchumi.
Kampuni hiyo pia imekuwa ikiunga mkono jitihada za serikali za kufikia malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) katika elimu kwa kutoa misaada mashuleni pamoja na taasisi za kijamii kama makanisa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni