Dar es Salaam.Taasisi ya Afya ya Ifakara kwa kushirikiana na ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa, wameamua kuanza kuchukua sampuli za damu za wagonjwa wanaohisiwa kuwa na maambukizi ya homa ya dengue na kwenda kuzifanyia vipimo katika ofisi ya Mkemia Mkuu.
Uamuzi huo umekuja kutokana na kuadimika kwa vipimo vya ugonjwa huo, sambamba na taasisi hiyo kumaliza muda wake wa kufanya utafiti kuhusu sababu za homa kwa mtu asiye na ugonjwa wa malaria.
Akizungumza jana, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Dk. Sophinias Ngonyani alisema katika kikao kilichofanyika jana na Mganga Mkuu wa Mkoa, ambacho walifikia maazimio kwamba sampuli za wagonjwa wenye viashiria vya dengue zichukuliwe kwa ajili ya vipimo katika maabara kuu ya taifa.
“Tumekaa kikao leo (jana) na Mganga Mkuu wa Mkoa, tumeazimia kwamba vipimo vitaendelea lakini kwa sasa tutachukua damu za wagonjwa na kupeleka maabara ya taifa, ambako zitapimwa na majibu yatarudi baada ya siku mbili. Hii inatokana na kumalizika kwa vipimo kutoka taasisi ya Ifakara Health Institute,” alisema Dk. Ngonyani.
Alisema umewekwa utaratibu maalumu jinsi ya kusafirisha sampuli hizo za damu kwa ajili ya kwenda kufanyiwa vipimo na kurudisha majibu yake baada ya kukamilika.
Ngonyani alisema kumalizika kwa utafiti huo, hakutaizuia taasisi hiyo kuendelea kutoa huduma kwani wamekwishaagiza vipimo vingine ambavyo vinatoka nje vinavyotarajiwa kuwasili keshokutwa.
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa homa ya dengue Dk. Mrisho Lupinda alisema utafiti wao ulikamilika Jumatano, lakini kutokana na ukubwa wa tatizo wataendelea na zoezi hilo.
“Kulingana na utafiti wetu, tulikuwa na namba kamili ya watu ambao tulihitaji kuwafanyia utafiti huu na namba hiyo ilishakamilika hapo ndipo tukamaliza zoezi letu, lakini tunaendelea na zoezi hili na Jumatatu. Vipimo vingine vitawasili ambavyo vimeagizwa nje ya nchi na tunaamini kwamba vitaendelea kusaidia wagonjwa mbalimbali wa homa hii,” alisema Lupinda.
Hata hivyo Lupinda alitoa wito kwa wagonjwa mbalimbali kukubali kupima vipimo vyote kwanza, kabla ya kukimbilia kipimo hicho kwani kina gharama kubwa.
“Kuanzia sasa mgonjwa yeyote atakayefika hospitali atalazimika kupima vipimo vyote ili tubaini iwapo ana malaria au homa ya aina nyingine, kabla ya kukimbilia kupima dengue. Hii itasaidia kuwa makini na kupunguza gharama ambayo ingeweza kupotea na gharama hiyo imfae mtu mwingine,” alisema Lupinda.
Gharama ya vipimo
Akielezea gharama za vipimo hivyo Dk. Ngonyani alisema vipimo hivyo vinakaa 25 katika pakiti moja ambavyo gharama yake ni kubwa ukilinganisha na vipimo vya malaria na ugonjwa mwingine.
1KUTOKA MWANANCHI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni