Dodoma.Mbunge wa Muhambwe (NCCR –Mageuzi), Felix Mkosamali amesema Kamati ya Bajeti ya Bunge haina kazi ya kufanya badala yake imegeuka pango la ufisadi na kupendekeza ifutwe mara moja kwa kuwa inawachanganya wabunge huku ikitafuna fedha za walipa kodi bila huruma.
Mkosamali alitoa tuhuma hizo juzi alipokuwa akichangia hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/15. Alisema kila inapokutana, wajumbe wake wanalipwa posho ya Sh500,000 kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ukilinganisha na wanacholipwa wajumbe wa kamati nyingine za Bunge.
Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge ambayo pia Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani (Wizara ya Fedha), ni mjumbe wake.
Wakati Mkosamali akitoa tuhuma hizo na kulitaka Bunge lifanye tathimini kama bado kuna haja ya kuwa na kamati hiyo, aliwatupia lawama wajumbe wake kwamba wanatengeneza mtandao wa rushwa kutoka kwa mashirika ambayo yanadaiwa kodi.
“Hakuna jipya katika kamati hiyo, sisi tumekaa humu ndani wao wako nje, wakija wanaanza kutuvuruga na hapa ninapozungumza wao wamejifungia huko na Tanapa eti wamewaita wajadiliane nao kuhusu ulipaji wa kodi, ni usanii mtupu kwani wanajadili nini wakati wameshawasilisha bajeti yao,” alisema.
Aliituhumu Serikali na wabunge wa CCM kuwa ni chanzo cha kuwafanya Watanzania waendelee kuishi katika umaskini uliotopea na kumpiga kijembe Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema amekuwa mtu wa kutoa kauli ambazo mwishowe anashindwa kuzisimamia.
“Mfano Waziri Mkuu alitoa kauli hapa kuwa atapunguza ununuzi wa magari ya VX, hakuna kilichofanyika na hakuna kitakachofanyika imebaki kuwatuliza watu, kwa nini isiletwe sheria hapa?” alihoji.
Alisema kauli ya kupunguza matumizi ya Serikali haijafanikiwa kwani imesababisha watu kubuni mbinu mbadala na hivyo kuendelea kutafuna fedha za umma bila ya huruma huku viongozi wengi wakitawaliwa na ubabaishaji.
Alitolea mfano wa sheria za Ghana kuhusu masuala ya ukopaji kwamba Katiba ya nchi hiyo inatoa nafasi kwa Bunge kujadili mkopo unaokopwa na namna utakavyotumika wakati Tanzania wanakaa watu wawili na kufanya uamuzi.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, Joseph Selasini alisema anayepaswa kulitolea majibu suala hilo ni Katibu wa Bunge au Mkosamali mwenyewe kutoa ushahidi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alipoulizwa alisema anayepaswa kulizungumzia ni Mkosamali mwenyewe ambaye naye alipoulizwa jana alisema maelezo yake yalikuwa sahihi kwa kuwa anavyo vielelezo vyote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni