KOCHA wa Simba, Patrick Phiri, ameangalia uchezaji wa straika Mbrazili wa Yanga, Genilson Santos ‘Jaja’ kwenye mechi dhidi ya Azam kisha akasema:“Huyu jamaa ni mfungaji, tuache unazi.”
Lakini Jaja mwenyewe akasisitiza kwamba mabao mawili aliyoichapa Azam yamempa mzuka wa hatari na kuanzia sasa atachapa kila timu na anaitamani sana mechi nyingine ngumu dhidi ya Simba itakayochezwa Oktoba 12 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam akisema ana uhakika wa kucheka na nyavu.
Jaja ambaye awali alikuwa akibezwa na mashabiki wakiwamo wa Yanga, alifunga mabao mawili juzi Jumapili wakati Yanga ilipoishinda Azam 3-0 katika mechi ya Ngao ya Hisani kwenye Uwanja wa Taifa. Bao jingine la Yanga lilifungwa na Simon Msuva.
Mchezaji huyo amefunguka na kuwaambia mashabiki watulie bado mambo matamu zaidi yanakuja na lengo lake ni moja tu kucheka na nyavu kila mechi kutetea heshima ya Yanga, lakini akawasisitiza kwamba wasitegemee mbwembwe nyingi kutoka kwake.
Alisema kwamba kazi yake ni kujiweka kwenye nafasi na kuhakikisha timu inashinda mambo mengine baadaye.
“Niliwaza siku nzima nikipanga nini nifanye uwanjani, nilijua kuwa naweza kupata nafasi lakini nilitaka kila nafasi mbili nitakazopata nizitumie, nafurahi kuona hilo limefanikiwa,” alisema.
“Sasa kwangu hali ya kujiamini imeimarika zaidi ilikuwa ngumu kuweza kuzoea mazingira haya ya hapa nchini kwa haraka, nikiendelea kuwa sawa kiafya nitafunga zaidi ya nilivyoifunga Azam, kila mechi ni magoli tu.
“Nataka mashabiki wafahamu kuwa soka ni mchezo wa kutumia akili, hivyo timu ama mchezaji inaweza kufanya makosa kila mara, cha msingi ni kuvumiliana na kupeana nafasi kwa kusapoti ili mambo yaende vizuri.
“Mimi binafsi nafanya makosa wakati mwingine, naweza hata kupoteza mpira na kuchukiwa, lakini lengo langu ni kupambana ili nifunge.”
Kocha Marcio Maximo alisisitiza: “Jaja amenipa furaha, amewafurahisha Wanayanga na pia ninawashukuru wachezaji wangu wote na benchi la ufundi kwa kazi waliyofanya. Nawaomba mashabiki waelewe kuwa Jaja si mchezaji wa mambo mengi, kazi yake ni kufunga na anacheza kwa nafasi, anakuwepo eneo la kufunga ambako ndiko anakotakiwa kucheza.”
Phiri afunguka Taifa
Phiri ambaye alilazimika kusafiri kwa ndege kuwahi mchezo huo akitokea Mtwara, alisema amemuangalia Jaja akicheza kwa dakika 80 na amegundua kwamba mshambulaiji huyo ni mchezaji hatari na jasiri ambaye hatakiwi kufanyiwa masihara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni