Dodoma.Makubaliano baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kutaka Bunge Maalumu lifikie ukomo Oktoba 4, mwaka huu yamezua sintofahamu mjinihapa huku uamuzi huo ukionekana kuwachanganya viongozi wa Bunge hilo.
Kutwa nzima ya jana, viongozi wa Bunge Maalumu walishinda kwenye vikao vya mashauriano huku wabunge wa CCM wakitarajiwa kukutana jana usiku kwenye makao makuu ya chama hicho kupewa taarifa rasmi za uamuzi huo.
Katika makubaliano baina ya TCD na Rais Kikwete, imeamuliwa kuwa uamuzi wa Rais kupitia Tangazo la Serikali (GN) 254 la kuongeza siku 60 hadi Oktoba 4 uheshimiwe na baada ya tarehe hiyo Bunge liahirishwe.
Uamuzi huo ni kinyume cha azimio la Bunge Maalumu la Agosti 5, 2014 ambalo lilirekebisha Kanuni ya 14 (4) na kuifuta Jumamosi katika siku zilizotajwa kuwa za kazi, pia sikukuu na siku za Jumapili.
Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alikaririwa akiwaambia wajumbe wa Bunge hilo kwamba Rais alikuwa ameridhia kwamba siku 60 alizotoa hazingejumuisha Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu.
Ni kwa msingi huo, Bunge hilo likapanga kwamba lingeendelea na shughuli zake hadi Oktoba 31, wakati Mwenyekiti wa Bunge atakapokabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais Kikwete.
Hata hivyo, makubaliano yaliyofikiwa baina ya viongozi wa TCD na Rais yanaonekana kuvuruga kabisa ratiba ya Bunge hilo ambalo jana na juzi, Kamati ya Uongozi ilikutana mara kadhaa kuona jinsi ya kunusuru mchakato huo.
Ingawa haikufahamika mara moja kama vikao hivyo vya kamati ya uongozi inayoongozwa na Sitta mwenyewe vinajadili nini, lakini taarifa zimedai huenda kukawa na mabadiliko makubwa ya ratiba.
Habari nyingine zinadai kwamba mabadiliko hayo huenda yakapunguza muda wa baadhi ya shughuli za kazi za Bunge hilo ili liweze kukamilisha kazi yake ikiwamo wajumbe kupiga kura ya uamuzi.
Katika kikao cha jana asubuhi, kamati hiyo ilishindwa kurekebisha ratiba yake ili iendane na siku zilizosalia, hivyo kuahirishwa kwa kuwapa kazi wataalamu wake kuleta mapendekezo ambayo yangejadiliwa jana mchana.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alithibitisha jana kwamba ratiba ya Bunge imebadilika kutokana na hoja nyingi kukubalika ndani ya kamati.
“Kamati ya uongozi itakutana baadaye (jana) kuangalia vipengele ambavyo hawakukubaliana kwenye kamati ndivyo wavipangie muda na ratiba itajulikana baada ya kikao hicho,” alisema Hamad.
Hofu ya akidi
Hata hivyo, habari zaidi zinadai kwamba uongozi wa Bunge Maalumu ulichanganywa na kuwapo kwa hoja za baadhi ya wajumbe wake kutaka kwenda Makka kwa ajili ya kushiriki Ibada ya Hijja, hali inayotishia akidi kwa ajili ya kuendesha vikao.
Kanuni za Bunge Maalumu zinataka kuwapo kwa nusu ya wajumbe kutoka pande zote za Muungano wakati wa kuendesha vikao vyake na theluthi mbili ya wajumbe hao kila upande wakati wa kufanya uamuzi au kupiga kura.
“Tumetoka kwenye kikao mchana huu na pengine tutaitana tena maana hatujafikia mwafaka, kuna mambo mengi yamejitokeza lakini kubwa ni hili la wenzetu ambao wanataka kwenda Hijja, kuondoka kwao kunaweza kuathiri akidi kwa kiasi kikubwa,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kamati hiyo.
Kutokana na matakwa hayo, hivi sasa Ofisi ya Katibu wa Bunge inafanya tathmini ili kufahamu idadi ya wajumbe ambao watakwenda Hijja Septemba 22, mwaka huu, ambao wengi wanatoka Zanzibar.
Hamad alikiri kwamba kuna mambo mengi ambayo ofisi yake inayafanyia kazi na kwamba hilo la Hijja ni mojawapo… “Kwa sasa siko katika nafasi ya kuzungumza kwa kirefu, kikao cha Kamati ya Uongozi kimeisha na bado kuna kazi nyingi za kuona jinsi tunavyoendelea.”
Tayari Bunge hilo limetikiswa na kutokuwapo kwa wajumbe waliosusia vikao tangu Aprili 16, mwaka huu ambao ni wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao unaundwa na vyama vya CUF, Chadema na NCCR Mageuzi na baadhi kutoka Kundi la 201.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni