Dodoma. Hatima ya Bunge Maalumu la Katiba imebaki mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete, ambalo limemwandikia barua kiongozi huyo wa nchi kutaka ufafanuzi wa kisheria kuhusu tarehe ya mwisho ya kumaliza vikao vyake.
Hiyo ni kutokana na muda uliopangwa kwenye ratiba ya bunge hilo kuzua utata wa kisheria na kuwapo uwezekano wa mwingiliano na Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi (BLW), Zanzibar.
Ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba inaonyesha kuwa limepanga kuhitimisha vikao vyake mwishoni mwa Oktoba, tofauti na tarehe iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete Julai 28, mwaka huu ambayo ilitangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 254 la Agosti Mosi.
Tangazo la Rais linaonyesha kuwa awamu ya pili ya Bunge Maalumu ingeanza Agosti 5, 2014 na kumalizika Oktoba 4, lakini ratiba ya Bunge hilo inaonyesha kuwa litamalizika Oktoba 31, siku ambayo mwenyekiti wa Bunge hilo atakabidhi kwa Rais Katiba inayopendekezwa.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hadi sasa Serikali bado haijatoa tangazo (GN) lingine kuongeza muda hadi mwishoni mwa Oktoba kama alivyosema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta wakati akitoa ufafanuzi wa siku 60 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo, Agosti 5 mwaka huu.
Sitta alisema kwa kadiri ya tafsiri, siku za kazi ni Jumatatu hadi Ijumaa ambazo wajumbe wanapaswa kufanya kazi na kwamba Jumamosi na Jumapili siyo sehemu ya siku 60 zilizoongezwa na Rais.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema hadi sasa hawajapata maelekezo ya ziada kutoka serikalini ambako waliandika barua ya kuomba ufafanuzi wa kisheria kuhusu suala hilo.
“Tulimwandikia barua, Katibu Mkuu Kiongozi (Ombeni Sefue) kuomba ufafanuzi wa siku hizo kama ambavyo sisi tungependa iwe, lakini hadi sasa bado hatujajibiwa lakini bado siku zipo nadhani tutajibiwa tu wakati mwafaka,” alisema Hamad ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi.
Sefue alikiri ofisi yake kupokea barua kutoka Bunge Maalumu ikiomba ufafanuzi ambao ungeliwezesha kuongeza siku kwa lengo la kukamilisha kazi ya kujadili na kuandika Katiba inayopendekezwa na kwamba maombi yao bado yanafanyiwa kazi.
“Bado tuna muda wa kutosha tu, ni kweli tulishayapokea maombi ya Bunge Maalumu kuhusu suala hilo na Mheshimiwa Rais akikamilisha kazi yake watajulishwa tu,”alisema Sefue.
Utata wa kisheria
Licha ya ahadi iliyotolewa na Sitta ni dhahiri kwamba suala hilo lina utata wa kisheria kutokana na kauli iliyowahi kutolewa na Mwanasheria wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema wakati akitoa ufafanuzi wa maana ya siku 70 ambazo Bunge lilikaa mara ya kwanza.
1 | 2 | 3
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni