Dar es Salaam.Wakati Serikali ikitupiwa lawama kwa kushindwa kumaliza tatizo la ajira kwa vijana nchini, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro amekiri kuwa Serikali haina uwezo wa kutoa ajira kwa vijana wote wanaohitimu masomo nchini.
Dk Migiro aliyasema hayo jana wakati alipofanya ziara katika Shule ya Sheria iliyopo jijini hapa na kuwataka vijana wanaomaliza vyuo kuweka kuweka mawazo kwenye upande wa pili wa ajira.
“Uchumi wa nchi yetu unajengwa na sekta binafsi katika maeneo mbalimbali…linaweza kuwa eneo la uchumi, biashara au taaluma kwa hivyo nategemea kwamba baadhi yenu mtaweka macho kwenye sekta binafsi…ni jambo zuri kwa sababu hivi sasa Serikali yetu, tofauti na sisi tuliyokuwa tunasoma haina uwezo wa kutoa ajira kwa wahitimu wote,” alikiri Dk Migiro.
Aliongeza: “Lakini wakati mtakapo kuwa kwenye sekta binafsi lazima mkumbuke kurejesha sehemu ya taaluma mnayopata hapa kwa jamii inayotuzunguka kwa kutoa huduma za kisheria pale zinapohitajika”
Alisema kuwa, serikali inategemea shule hiyo itazalisha makada wenye malezi bora na wenye ufanisi mzuri wa taaluma ya sheria ambao wataweza kumudu ushindani uliyopo kwenye fani hiyo kutoka kwa wanasheria wenzao wanaotoka nje ya nchi.
“Tunaamini kwamba mafunzo kwa vitendo wanayopata wanafunzi hawa kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kuhitimu shahada ya sheria katika vyuo mbalimbali nchini yatawajengea uwezo mzuri na ufanisi wa kuwa mawakili wazuri,”alisema Dk Migiro.
Akizungumzia changamoto ya gharama za mafunzo, waziri huyo alisema kuwa serikali imekwisha peleka mswada bungeni ili sheria inayoruhusu wanafunzi wa elimu ya juu kunufaika na mkopo iweze kuongezwa sehemu ya wanafunzi wa shule ya sheria pia.
“Muswada ukifanyiwa kazi tunategemea ndani ya miaka miwili wanafunzi wanaosoma shule ya sheria nao wataanza kupata mikopo. Nimesikia kuna baadhi wanashindwa kuendelea na shule ya sheria kutokana na changamoto za kifedha hivyo tunashughulikia hilo tatizo,”alisema na kuongeza
“Licha ya kuwa mkopo huo unaweza usitosheleze kwa asilimia mia, lakini utasadia…wazazi na walezi nao ningeomba wajitahidi kupunguza gharama za matumizi yasiyo na manufaa kwa watoto wao na badala yake wajitahidi kuwekeza zaidi kwenye elimu.”
MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni