Kurasa

Ijumaa, 24 Oktoba 2014

KIKWETE ATAMANI MUDA WA KUSTAAFU URAIS UFIKE

RAIS Jakaya Kikwete amesema mfumo unaotumika Tanzania ambako Rais anatumikia nafasi ya uongozi kwa muhula wa miaka mitano na si zaidi ya miaka 10 ni mzuri na unaovutia kwa sababu unaiwezesha nchi kupata fikra na mawazo mapya.
Aidha, Rais Kikwete amesema, anaamini Tanzania itapata Rais bora zaidi kuliko yeye, atayeiwezesha Tanzania kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi.
Rais Kikwete pia amesema, ana hamu kumaliza muda wake wa uongozi ili arudi kijijini kushughulika na wajukuu wake na mifugo yake. Rais Kikwete ametoa kauli hiyo mjini Beijing, China, wakati akizungumza na mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika China.
Mkutano huo uliofanyika kwenye Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali ya China ya Diaoyutai, ulikuwa shughuli ya kwanza ya Rais Kikwete katika ziara yake rasmi ya siku sita ya Jamhuri ya Watu wa China ambako amealikwa na Rais Xi Jinping.
Wakati wa maswali na majibu, Balozi Sola Onadipe, Naibu Balozi wa Nigeria katika China, alishangazwa na kauli ya Rais Kikwete kuwa anatamani amalize muda wake wa uongozi ili astaafu na kusema kuwa lingekuwa jambo la maana kwa Afrika kama viongozi wengine wangekuwa na mawazo ya namna hiyo ya kuheshimu Katiba za nchi zao na kung’atuka kwenye uongozi muda wao unapowadia.
Rais Kikwete amemwambia Balozi huyo:”Ni kweli naona kama muda hauendi kwa kasi ya kutosha ili niweze kuwa raia wa kawaida na nipate muda wa kuchunga ng’ombe na mbuzi wangu na nilime mananasi yangu kwa nafasi ya kutosha. Lakini Mheshimiwa Balozi usishangazwe na utayari wangu kuondoka katika uongozi.”
“Kwanza utaratibu huu wa miaka mitano ama miaka 10 ni utaratibu wa Kikatiba, ni jambo lililoko katika Katiba yetu na hatuna kishawishi cha kulibadilisha. Pili, kazi hii ya Urais ni kazi ngumu sana. Kwa hakika, binafsi nawaonea gele sana wenye nguvu na ubavu wa kutaka kubakia kwenye kazi hii kwa miaka mingi. Pengine wana nguvu zaidi kuliko mimi,”amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“ Lakini pia kuna uzuri katika mfumo huu wa kwetu kwa sababu kila baada ya miaka mitano na hata kama ni baada ya kila miaka kumi, anaingia mtu mwingine madarakani akiwa na fikra mpya na mawazo mapya.”
“Mfumo huu ni mfumo unaoniridhisha sana na wala hakuna kinachonishawishi nibakie katika madaraka zaidi ya muda wangu kikatiba. Nina hakika, nchi yetu itapata kiongozi mwingine, bora kuliko hata mimi, kuongoza vizuri nchi yetu.”
Rais Kikwete pia amesema kuwa si busara pia kwa kiongozi kuwasikiliza wale wanaoshauri wakisema kuwa akiondoka madarakani nchi itavurugika.
“Kwa hakika, hawa wanatetea maslahi yao tu wakisema kuwa ukiondoka wewe madarakani, wao hawatakuwa tena mabalozi ama mawaziri ama nafasi nyingine yoyote.”
mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni