Kurasa

Ijumaa, 13 Juni 2014

WAHITIMU 10000 WAFANYIWA USAILI KWA NAFASI 70 ZA KAZI

Wasomi 10,500 wasailiwa uwanja wa Taifa kujaza nafasi 70 tu za Uhamiaji.......
6/14/2014 habari za kitaifa
Katika hali inayoashiria ukubwa wa tatizo la ajira katika sekta rasmi nchini, wasomi wa ngazi ya Chuo Kikuu 10,500 walijitokeza jana (pichani) kwenye usaili wa Idara ya Uhamiaji nchini inayohitaji kuajiri watu 70 tu.
Wengi wakiwa ni vijana wasomi wa fani mbalimbali wenye umri wa kati ya miaka 22 na 30, walifurika kwenye uwanja huo uliopo Kurasini, katika Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam kuanzia saa 12 asubuhi.
Idadi hiyo inahusisha waombaji wa ajira walioitwa na idara hiyo kutoka kundi la waombaji 20,000.
Idadi ya waombaji hao walijiotokeza katika usaili huo ilithibitishwa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isack Namtanga, aliyekiri ni usaili wa kihistoria kutokana na kuhusisha waombaji wengi kwa wakati mmoja.
“Kwa kweli huu ni usaili wa kihistoria, hatujawahi kupata maombi mengi kama haya, wote waliotuma ni wale wenye sifa kielimu ambayo ni kuwa na shahada ya kwanza ya fani tulizozitaja hapo awali,”alisema.
Alifafanua kuwa, Wizara kupitia matangazo ya nafasi hizo za ajira katika vyombo vya habari yaliyotolewa mapema mwanzoni wa mwaka huu, yaliainisha nafasi zinazohitaji watu na sifa zake ambapo katika nafasi ya kwanza ni ya Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji iliyohitaji watu 70.
Sifa za nafasi hiyo ni pamoja na waombaji kuwa na elimu ya Shahada ya Kwanza katika fani za Uchumi, Biashara, Utawala, Uandishi wa Habari, Ualimu, Usafirishaji, Rasilimali Watu na Sayansi ya Kompyuta.
Nyingine ni Habari na Mawasiliano, Takwimu, Uchapaji, Uhandisi Majengo na Uhandisi Mitambo.
“Na masharti yalitaka waombaji hao wawe na umri usiozidi miaka 35, jambo ambalo waombaji wote 20,000 waliotuma maombi yao walikuwa na sifa hizo hivyo ikabidi wachujwe ili kupata waombaji watakaoitwa kwenye usaili.
“Hii inaonesha kuna uhaba mkubwa wa ajira, na waombaji wote wana sifa hiyo ya shahada na umri, sasa tulifanya usaili kwa makini tukapata hao zaidi ya 15,000 tumejitahidi na tumewaita wengi ili waje wachuane kwenye usaili tupate hao 70,”alisema Namtanga.
Akizungumzia jinsi watakavyopata waombaji wenye sifa ikiwa wote waliotuma maombi wanasifa tajwa, Namtanga alisema pamoja na kuangalia sifa ya elimu, lakini pia wataangalia na ufahamu wa mambo mengine ya kijamii.
Alisema hiyo ni ili kupata waombaji wenye upeo mkubwa hasa kwa kuwa wengi wao wana sifa kielimu, hivyo kuitwa kwao kwa wingi ni kutoa mwanya kwa wao kuchuana kwa uwazi na kupata waombaji kwa haki.
Kwa upande wa waombaji hao, baadhi ya waliozungumza na gazeti hili baada ya kutoka kwenye usaili huo walisema, ni usaili mgumu kwani una ushindani wa hali ya juu.
“Sijawahi kufanya usaili wa watu wengi kama huu, nafasi zinazohitajika ni 70, ila tulikuwa zaidi ya 10,000 sasa unaona wazi kwamba ni lazima ufanya kwa makini ili kushindania nafasi hizo”,alisema mmoja wa waombaji hao ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Aliongeza, hali hiyo inaonesha jinsi gani vijana wengi wana uhaba wa ajira, kwani kwa nafasi hizo 70, maombi ni mengi na yanavunja historia ya usaili wa nafasi nyingine mbalimbali zilizowahi kutangazwa.
Alisema katika usaili huo, waliufanya kwa kugawanywa kwenye makundi mawili, ambapo walitumia Uwanja wa Taifa kufanyia kwa kuketi kwenye viti vya watazamaji mithili ya waliokuwa wanaangalia pambano la soka kwenye uwanja huo wa kisasa wa michezo nchini.
Kuhusu usimamizi na ulinzi wakati wa usaili, mmoja wa wasaili hao alisema wasimamizi walikuwa wa kutosha wakiongozwa na Maofisa kutoka Uhamiaji, Magereza na baadhi ya maofisa kutoka Utumishi.
“Usimamizi ulikuwa mzuri na walikuwepo wasimamizi wa kutosha, tulifanya kwa makundi mawili moja lilikuwa chini uwanjani na wengine walipanda juu kwenye jukwaa la watazamaji, tulifanya mtihani wa kuandika, ulikuwa mzuri tu, ndio tusubiri tuone majibu,”alisema mmoja wa waombaji hao aliyeshukuru magazeti na vyombo vya habari kwa ujumla kwa mchango wao mkubwa katika kuihabarisha jamii juu ya masuala mbalimbali ikiwa pamoja na nafasi za ajira zinazotangazwa.
Hata hivyo Namtanga alisema , baada ya usaili huo kukamilika, watafanya uchambuzi na watachagua watu waliofanya vizuri kwa ajili ya usaili wa pili wa kuzungumza.
“Tumejipanga vizuri, tunategemea kazi hii itafanyika kwa utulivu na tutapata watu wenye sifa na ufahamu wa mambo ya kijamii kwani ni moja ya sifa ya ziada,”alisema Namtanga.
Alisema watakaopata nafasi hizo watakuwa na majukumu mbalimbali yakiwemo kusimamia doria sehemu za mipakani, bandarini vituo vya mabasi, kusimamia shughuli za upelelezi, kuandaa hati za mashtaka, kukagua na kusimamia hati za safari na majukumu mengineyo.
Wakati wasomi hao wakionesha kiu ya ajira katika sekta rasmi, katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikisisitizwa umuhimu wa wasomi kujiajiri kutokana na ajira rasmi kuwa na nafasi chache, si kwa Serikali ya Tanzania pekee, bali kote duniani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni