Kurasa

Jumamosi, 25 Oktoba 2014

HALMASHAURI YA WILAYA YA BAGAMOYO TABIA HII INASABABISHA WANAFUNZI KUFELI

Wilaya ya Bagamoyo ni moja kati ya wilaya za mkoa wa pwani zinazofanya vibaya katika matokeo ya kidato cha nne na hivyo kusababisha wanafunzi kutangatanga na wengine kuishia kupata ujauzito na kuolewa.

Zimekuwa zikisemwa sababu nyingi zinazochangia wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao na nyingi ya sababu hizo zimekuwa ni lawama kwa upande wa serikali kuu na walimu huku sababu ndogondogo ambazo zinahusiana moja kwa moja na wanafunzi wenyewe na wazazi zikiachwa na hivyo kuendelea kurudisha nyuma ufanisi wa wanafunzi.

Moja kati ya sababu hizo ni hii inayofanywa na serikali ya halmashauri ya wilaya ya bagamoyo ya kutoa vibali kwa watu kufanya sherehe zao za harusi au nyingine usiku katikati ya makazi ya watu huku ukipigwa muziki mzito ambao husababisha kelele na kero kwa majirani.

Mbaya zaidi ni kwamba wanafunzi wamekuwa wakitoka katika nyumba zao na kwenda kucheza rusha roho katika sherehe hizo na kuacha jukumu lao la kujisomea na hasa ukizingatia kuwa hawawezi tena kusoma kutokana na kelele zinazoendelea.

Kama hiyo haitoshi sherehe hizo zinakuwa ni fulsa kwa vijana waharibifu kuwarubuni wanafunzi wa kike na kuwaingiza katika vitendo vya kufanya mapenzi wakiwa bado wanafunzi.

Kinachokera zaidi ni kwamba mbali na Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo kutokukemea tabia hizo imekuwa namba moja kutoa vibari vya kuruhusu watu kufanya sherehe hizo katika makazi ya watu huku wakijua fika kuwa kuna kumbi maalum kwaajiri ya kufanyia sherehe hizo na sio katika makazi ya watu.

Ombi langu kwa serikali ya Halmashauri ya Bagamoyo na serikali za halmashauri zote nchini ni kuwa tusishirikiane kuendelea kulitengeneza bomu hili ambalo tunaona kabisa kuwa mwisho wake sio mzuri.

Hawa tunaowaita sasa hivi watoto wa uswahilini tukumbuke kuwa ni wengi sana na miaka kadhaa ijayo tutakuwa tumezalisha kundi kubwa sana la watu wasiokuwa na elimu na ambalo bado litakuwa na mahitaji na hivyo kusababisha vitendo vya wizi na ujambazi kuongezeka.

Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo mnapaswa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake mbadilike na kutimiza majukumu yenu ipasavyo bila kutengeneza mbonu za kujikinga huku mkijua fika kuwa kizazi hiki na vijavyo vinategemea sana busara na fikra sahihi za ki uongozi kutoka kwenu.

Matumaini yangu ni kuwa wahusika mala baada ya kuwakumbusha hapa mtachukua hatua stahiki badala ya kuanza kuwa na mawazo hasi ya kutafuta mchawi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni