Kurasa

Jumapili, 26 Oktoba 2014

SALE YA TANO MFULULIZO YAMLIZA OKWI

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Anord Okwi na kipa chupukizi Manyika Peter Jr, jana walimwaga machozi baada ya timu yao ya Simba kutoka sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine, mjini hapa.
Nyota hao walifanya hivyo baada ya mwamuzi wa mechi hiyo, Athumani Lazi kutoka mkoani Morogoro kupuliza filimbi ya mwisho kumaliza pambano hilo namba 33.
Kilichowaliza Okwi na Manyika Jr katika mechi hiyo, ni kuona timu yao ikiambulia sare kwa mara ya tano licha ya hiyo jana kuwa mbele katika kwa dakika 78, baada ya wao kupata bao kuongoza dakika ya nane.
Bao hilo lilifungwa na Okwi kwa mpira uliotokana na na adhabu ndogo na kwenda moja kwa moja wavuni na kumwacha kipa Mohamed Yusuph akiwa hana la kufanya.
Licha ya maafande wa Tanzania Prisons chini ya Kocha David Mwamwaja kupambana kusawazisha bao hilo, Simba walikuwa makini na kwenda mapumziko wakiwa mbele.
Kipindi cha pili maafande wa Prisons walionekana kuimarika wakifanya mashambulizi ya uhakika na kujilinda vizuri na kupata bao dakika ya 86, likifungwa na Hamis Maingo aliyeingia kipindi cha pili akiubetua mpira kwa juu wakati huo kipa Manyika Jr akiwa ametoka langoni.
Baada ya filimbi ya mwisho, ndipo Okwi alikaa chini na kuanza kulia hadi aliposaidia na wachezaji wenzake kwa kumnyanyua kama ilivyokuwa kwa Manyika Jr ambaye alifarijiwa na kipa namba moja wa timu hiyo, Ivo Mapunda.
Tangu kuanza kwa ligi hiyo msimu huu, ni sare ya tano kwa Simba kwani jana walishuka dimbani wakitoka kuvuna matokeo ya aina hiyo kwa Coastal Union, Polisi Moro, Stand Utd na Yanga.
Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi tano katika mechi tano tangu kuanza kwa ligi hiyo Septemba 20 huku Tanzania Prisons nao wakifikisha pointi kama hizo.
Wakati Simba ikizidi kuchechemea, watani wao Yanga jana wakicheza katika Uwanja wa Kambarage, mkoani Shinyanga, jana walivuna pointi tatu katika mbio za ligi hiyo baada ya kuinyoa Stand Utd mabao 3-0, anaripoti Mwandishi Wetu Stella Ibengwe.
Yanga chini ya Mbrazil Marcio Maximo, walipata bao la kwanza dakika ya 13, likifungwa na Jaja na kudumu hadi filimbi ya mapumziko.
Kipindi cha pili, kiliendelea kuwa cha mashambulizi makali ambapo wakati Yanga wakipambana kuongeza mabao, wenyeji Stand Utd nao walikuwa wakitaka kusawazisha bao hilo.
Lakini, mtokea benchi Jerrison Tegete aliyeingia kuchukua nafasi ya Jaja, aliifungia bao la pili katika dakika ya 79 na kuamsha umati wa wapenzi na mashabiki wa Yanga waliokuwa wamejitokeza kushuhudia mechi hiyo.
Dakika ya 90, Tegete kwa mara ya pili alirejea katika nyavu za Stand Utd na kuifungia timu yake bao la tatu, hivyo kufikisha pointi 10 katika mechi tano tangu kuanza kwa ligi hiyo.
Wakati Yanga wakifikisha pointyi hizo, Stand United moja ya timu ngeni katika ligi hiyo ikicheza kwa mara ya kwanza, wameendelea kupotea katika ligi hiyo wakiambulia pointi tano katika mechi tano.
Nayo Azam FC ikicheza katika Uwanja wake wa Azam Complex, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, jana walichapwa bao 1-0 na maafande wa JKT Ruvu ya Pwani, anaripoti Mwandishi Wetu Salum Mkandemba.
Bao la JKT Ruvu chini ya kocha wake Fred Felix Minziro, lilifungwa dakika ya 45 na mtokea benchi, Samuel Kamuntu akichukua nafasi ya Idd Mbaga aliyeumia na kuwainua mashabiki wa timu yake iliyoshuka dimbani ikitoka kuwafunga Tanzania Prisons katika mechi iliyopita.
Kamuntu alifunga bao hilo akiunganisha krosi murua ya Najimu Magulu kutoka wingi ya kulia, maafande hao wakisawazisha makosa ya dakika ya 40, waliposhindwa kuitumia vizuri nafasi baada ya Magulu kushindwa kuitendea haki pasi ya Ally Bilali.
Kipindi cha kwanza kilikuwa cha soka ya nguvu huku pengo la Kipre Tchetche kwa upande wa Azam FC, likionekana bayana kwa upande wa Azam FC kwani Didier Kavumbagu alionekana mara nyingi kukosa sapoti.
Katika kipindi cha pili, Azam waliongeza kasi kwa lengo la kusawazisha bao hilo, lakini maafande wa JKT Ruvu nao wakipambana kulinda na kushambulia na hadi mwisho, JKT Ruvu walifanikiwa kuondoka na ushindi wa bao 1-0.
Kwa ushindi huo, JKT Ruvu wamefikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tano huku mabingwa watetezi, Azam FC wakibaki na pointi zao 10. Kwa upande mwingine, ni kipigo cha kwanza kwa Azam katika Ligi Kuu Tanzania bara, baada ya mechi 37 zilizopita.
Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa mechi kadhaa kwa timu kuzidi kupigania pointi kujiongezea mtaji katika kuuwania ubingwa wa ligi hiyo unaoshikiliwa na Azam tangu April 19, 2014.

TANZANIA DAIMA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni