Kurasa

Alhamisi, 18 Septemba 2014

KINGUNGE ATAKA WAFANYAKAZI WASIFANYE BIASHARA

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru, ameitaka Serikali kutunga sheria itakayowabana wafanyabiashara wanaojiingiza kwenye siasa na kugombea uongozi kujitenga na biashara zao kwa kipindi chote wanachofanya kazi za utumishi wa umma ili kuimarisha uadilifu wa viongozi.
Kingunge aliyasema hayo wakati wa mahojiano maalumna NIPASHE mjini Dodoma na kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa pamoja na namna ya kukabiliana nazo.
Alisema kuwa biashara ni muhimu sana katika maisha ya binadamu, lakini na uongozi pia ni muhimu, hivyo mtu akichanganya mambo hayo na kuyafanya kwa wakati mmoja, lazima kutatokea madhara kwa jamii anayoitumikia.
Alisema kwa kawaida lengo kubwa la kufanya biashara ni kupata faida wakati kwa upande wa uongozi kazi kubwa ni kufanya maamuzi yenye maslahi kwa jamii, hivyo mtu akijihusisha na mambo hayo mawili kwa wakati mmoja kinachotokea kwa upande wa uongozi ni kutumia madaraka kwa maslahi binafsi.
“Ukichanganya uongozi na biashara utapata mambo makubwa mawili, kwanza hutakuwa na muda wa kutosha wa kufanya kazi za wananchi huku ukijihusisha na biashara zako, badala yake utafanya nusu nusu na kutokana na mvuto wa fedha, akili yako yote itaishia kwenye biashara,” alisema Kingunge ambaye ni mfuasi mzuri wa itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea.
Alisema kutokana na watu wengi hivi sasa kukosa uzalendo kwa nchi yao, umefika wakati ambao sasa taifa linapasa kuchukua hatua kwa kutenganisha kabisa shughuli za uongozi na biashara.
Alisema kinachopaswa kufanyika ni kutunga sheria ambayo itamlazimu mtu yeyote anayetaka kuwania nafasi za juu za uongozi wa taifa kwanza kutangaza mali zake na kisha kujitenga nazo kwa kipindi chote anachotumikia umma.
“Uwekwe utaratibu ambao mtu akishachaguliwa kuwa kiongozi wa umma, akabidhi kisheria mali au biashara zake kwa mtu au kampuni iziendeshe na yeye asijihusishe nazo kabisa mpaka atakapokuwa amemaliza muda wake wa uongozi,” alisema Kingunge.
Alisema kuwa chimbuko la mahitaji ya sheria ya aina hiyo ni kuporomoka kwa uzalendo miongoni mwa Watanzania hususan viongozi kubainika kuwa wanaweka mbele maslahi yao zaidi kuliko maslahi ya umma na taifa kwa ujumla.
Mwaka 2008 kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichofanyika Butiama, mkoani Mara, Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, pia alizungumzia suala la kutenganisha uongozi na biashara.
Suala hilo lilizua mjadala mkali miongoni mwa wajumbe na baada ya kikao, muingoni mwa maazimio yaliyosomwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, ni kutenganisha uongozi na biashara.
Ingawa tamko hilo maarufu kama Azimio la Butiama kueleza kuwa iingetungwa sheria ya kaainisha suala hilo ili liwabane wanasiasa wa vyama vyote vya siasa, hadi leo sheria hiyo haijatungwa na wanasiasa wengi ni wafanyabiashara.
AZUNGUMZIA UBINAFSI
Kingunge pia alielezea jinsi ambavyo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alivyojitahidi kukabiliana na tabia ya ubinafsi hata kabla ya nchi kupata Uhuru.
Kingunge alisema kuwa tabia ya ubinafsi miongoni mwa Watanzania lilianza miaka ya 1960 baada ya kuonekana kuwa kuna dalili ya Uhuru kupatikana na kwamba ilibidi Watanzania waanze kujipanga namna watakavyoendesha taifa lao baada ya kujipatia Uhuru.
Alisema kabla ya wakati huo hapakuwapo ubinafsi ndani ya Tanu kwa kuwa watu wote walikuwa na nia moja tu ya kuhakikisha wanamng’oa mkoloni.
Alisema Uhuru ulipokaribia iliwabidi waanza kujipanga na kugawana vyeo ndani ya chama na serikalini, hali ambayo ilisababisha kuanza kwa ubinafsi nchini kutokana na watu kuhitaji madaraka na vyeo vikubwa.
Alisema hali ilianza kuwa mbaya zaidi baada ya Uhuru kupatikana, kwa kuwa watu walihitaji kujilimbikilizia vyeo na mali, kitu ambacho kilimsukuma Mwalimu Nyerere kuanzisha Azimio la Arusha kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo.
“Kwa kuona hali inazidi kuwa mbaya, Mwalimu Nyerere akaanzisha Azimio la Arusha na ndiyo sababu unaona ndani ya Azimio la Arusha kuna miiko ya kuzuia viongozi kujineemesha wenyewe,lakini pamoja na kuwapo kwa Azimo la Arusha, bado ubinafsi ulikuwapo, kwa kweli tulishindwa kabisa kumaliza tatizo hili,” alisema Kingunge ambaye ameshika nafasi za kichama na serikali katika awamu zote nne za uongozi.
Kingunge, alisema baada ya kuvunjika kwa Azimio la Arusha, viongozi wa umma walianza kuonyesha ubinafsi wao wazi wazi huku wakishambulia mashirika na mali nyingine za Umma, hali iliyopelekea Serikali kutunga sera ya ubinafsishaji wa mali za umma ili kunusuru mali za umma na kurejesha uzalendo.
Hata hivyo, alisema ubinafsishaji haukusaidia kurejesha uzalendo kwa Watanzania na badala yake uliudhoofisha zaidi kwa kuongeza ubinafsi na tamaa ya viongozi kujilimbikizia mali.
Alisema mbaya zaidi katikati ya ubinafsishaji huo likaingia suala la rushwa ambalo pia liliongeza ukubwa wa tatizo na kusababisha wanyonge kushindwa kufaidi matunda ya taifa lao.
“Rushwa na ubinafsi ulianzia kwenye sekta ya uchumi, ukaingia kwenye huduma za kijamii na sasa unaelekea kwenye siasa, lakini tutambue kuwa siasa ni muhimu sana katika kuendesha huduma za kijamii, ubinafsi ukiingia huko siasa itakuwa kama biashara na hapo hali itazidi kuwa mbaya zaidi,” alionya Kingunge na kuongeza:
“Kutokana na kutoweka kwa uzalendo na uadilifu miongoni mwa viongozi, kwa sasa watu hawaendeshi mambo kwa unyoofu wala usawa, badala yake wanaongozwa zaidi na msingi wa mimi nitapata nini katika hili, suala la kujitolea sasa hivi halina nguvu.”
Alisema kutokana na hali hiyo, ndiyo sababu kuna umuhimu wa Serikali kutunga sera na sheria zinazombana kiongozi ajitenge na mali pamoja na biashara zake kwa kupindi chote anachotumikia wananchi kwa lengo la kudhihirisha suala la uadilifu.
Katika toleo la kesho, Kingunge ataendelea kuzungumzia mambo mbalimbali ikiwamo suala la elimu na changamoto zake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni