Kurasa

Ijumaa, 1 Agosti 2014

MTANDAO WA ULIPUAJI WA MABOMU ARUSHA WANASWA

Mtanzania
WATU 19 wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha, wakidaiwa kuhusika na uingizaji, ulipuaji na usafirishaji wa mabomu pamoja na kumwagia watu tindikali.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kununua mabomu hayo Jamhuri na Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, kililiambia MTANZANIA kuwa watuhumiwa hao akiwamo Sheikh wa Msikiti wa Bondeni jijini hapa na mfanyakazi wa Benki ya Stanbic, walitiwa mbaroni na Jeshi la Polisi baada ya kufanya uchunguzi uliowezesha kunasa mawasiliano ya simu pamoja na mitandao ya kijamii.
Chanzo hicho kilisema kuwa, watuhumiwa hao hutumia madereva wa bodaboda kwenda kununua mabomu hayo na kuyapitisha kwenye mpaka wa Burundi na Tanzania wa Manyovu mkoani Kigoma.
Chanzo hicho kilieleza kuwa mabomu hayo na tindikali husafirishwa na mabasi hadi mkoani Arusha ambapo hutumika kwenye vitendo vya kihalifu.
Watuhumiwa hao wote kwa pamoja wanapandishwa kizimbani leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kujibu tuhuma zinazowakabili.
Habari zaidi zilidai kuwa mtuhumiwa mwingine, Yahaya Hassan Hela maarufu kama Sensei, ambaye ni kinara wa matukio hayo anaendelea kusakwa.
Hivi karibuni jeshi hilo liliwakamata watuhumiwa wengine sita na kuwafikisha mahakamani kuhusiana na mlipuko wa bomu uliotokea Julai 7, mwaka huu kwenye Mgahawa wa Vama eneo la Viwanja vya Gymkhana jijini Arusha.
Katika operesheni hiyo mkazi wa Sombetini, Yussuf Hussein Ali na mkewe, Sumai Yussuf Ali, waliokutwa wakiwa na mabomu saba ya kurusha kwa mkono, risasi sita na unga wa baruti vikiwa nyumbani kwao, nao watafikishwa mahakamani leo kujibu tuhuma hizo.
Akizungumzia operesheni iliyofanikiwa kunasa watuhumiwa 19, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema ushahidi uliokusanywa umebaini kati yao watuhumiwa 21 wanahusika na matukio ya ulipuaji mabomu na umwagaji wa tindikali jijini Arusha.
“Matukio hayo ni yale yaliyotokea mwaka 2012 na hivi karibuni. Watuhumiwa hawa wanatazamiwa kufikishwa mahakamani kesho (leo), kuungana na wenzao waliokwishatangulia ili kujibu mashtaka,” alisema Kamanda Sabas.
Kamanda Sabas aliwataja watumiwa waliokamatwa na matukio waliyohusika nayo kama ifuatavyo:-
Bomu nyumbani kwa Katibu wa Bakwata
Kamanda Sabas aliwataja waliohusika na tukio la ulipuaji wa bomu nyumbani kwa Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania Mkoa wa Arusha, Sheikh Abdulkarim Jonjo Oktoba 25, mwaka 2012 ni Yussuph Ally Huta (30), Kassim Ramadhan (34).
Wengine ni dereva wa bodaboda, Mustapha Mohamed Kiago (49) pamoja na Sheikh wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa, Abdulaziz Mohamed (49) ambaye pia alikuwa Imamu wa msikiti huo.
Kanisa la Olasiti
Aliwataja waliohusika na tukio la ulipuaji wa bomu kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi la Olasiti jijini Arusha Mei 5, mwaka 2013, kuwa ni Yusuph Huta (30), Ramadhan Waziri (28), Abdul Humud (30) na Wakala wa Mabasi ya Mohamed Trans (ambaye amefikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na bomu la Mgahawa wa Vama).
Wengine ni Jafar Lema (38), ambaye alikuwa Imamu wa Msikiti wa Quba (ambaye amefikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na bomu la Mgahawa wa Vama), Said Mohamed Temna (42), (ambaye amefikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na bomu la Mgahawa wa Vama).
Wengine ni Kassim Ramadhan (34), Abashar Omar (24), ambao ni madereva bodaboda, Abdulrahman Hassan (41), pamoja na mfanyakazi wa Benki ya Stanbic Arusha.
Wengine ni Morris Muzi (44), mkazi wa Kalinzi mkoani Kigoma, Niganya Niganya (28), mkazi wa Businde Ujiji Kigoma, Baraka Bilango(40), mkazi wa Kalinzi Kigoma na Hassan Omar (40).
Mlipuko mkutano wa Chadema
Alisema Jeshi la Polisi limewanasa watuhumiwa kadhaa ambao walihusika katika tukio la ulipuaji wa bomu Juni 15, mwaka jana kwenye mkutano wa kampeni za udiwani za Chadema.
Watuhumiwa hao ni Yusuph Huta (30), Abdul Humud (30), pia wapo Said Temba (42), ambao wamefikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na bomu la Mgahawa wa Vama na Jafar Lema (38).
Wengine ni Imamu wa Msikiti wa Quba, Sheikh Abuu Ismail, ambaye amefikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na bomu la Mgahawa wa Vama.
Wengine ni Kasim Ramadhan (34), ambaye ni dereva wa bodaboda, Ramadhan Waziri (28).
Alitaja watuhumiwa wengine kuwa ni Abashar Hassan Omar (24), Abdulrahman Hassan (41), mfanyakazi wa Benki ya Stanbic Arusha, Morris John Muzi (28).
Wengine ni Niganya Niganya (28), Baraka Bilango (40) na Hassan Omar (40).
Kumwagiwa tindikali Sheikh Makambawa
Katika tukio la Julai 11, mwaka jana la kumwagiwa tindikali Sheikh Said Makambawa wa Msikiti wa Morombo, Kamanda Sabas aliwataja watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo kuwa ni Yusuph Ally (30), Ramadhan Waziri (28), Kassim Ramadhan (34) na Jafar Lema (38) aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Quba.
Kumwagiwa tindikali Sheikh Mustapha
Katika tukio hilo lililotokea Februari 28, mwaka huu, watuhumiwa katika tukio hilo ni Yusuph Ally (30), Kasssim Ramadhan (34), Jafar Lema (38) na aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Quba na Hassan Mfinanga (57).
Tukio la Arusha Night Park
Katika tukio hilo lililotokea Aprili 13, mwaka huu, watuhumiwa ni Jafar Lema (38), Imamu wa Msikiti wa Quba, Ibrahim Lenard au Sheikh Abuu Ismail (37) ambao wote walifikishwa mahakamani.
Bomu nyumbani kwa Sheikh Sudi
Kamanda Sabas aliwataja watuhumiwa waliorusha bomu kwa Sheikh Sudi, Julai 3, mwaka huu kuwa ni Yahaya Twalib (37), Idd Yusuph (32), Said Temba (42) ambaye amefikishwa mahakamani kwa kuhusishwa na bomu la Mgahawa wa Vama.
Wengine ni Anwar Nasher Hayel (29), Jafar Lema (38) ambaye amefikishwa mahakamani, Hassan Mfinanga (57), Yusuph Ramadhan (23) na Abashar Omar (24).
Tukio la mabomu nyumbani
Alisema katika tukio hilo la Julai 21, la familia kukamatwa na mabomu saba, watuhumiwa ni Yusuph Huta (30) na mkewe Sumaiya Yusuph Ally (19), Ramadhan Waziri (28), Hassan Ally Mfinanga (57) na Abashar Hasan Omar (24) ambaye ni dereva bodaboda.
Wengine ni Kimoro Mcahan (25), Hassan Omar (40), Morris Muzi (44), Niganya Niganya (28), Muha na mkazi wa Businde Ujiji mkoani Kigoma na Baraka Ntembo Bilango (40) Muha na mkazi wa Kalinzi Kigoma.
Kosa la kuhamasisha ugaidi kwa mtandao
Alisema jeshi hilo linawashikilia baadhi ya watuhumiwa kwa kuhusika na kosa la kuhamasisha vitendo vya kigaidi kupitia mitandao ya kijamii.
Watuhumiwa hao ni Ibrahim Lenard au Sheikh Abuu Ismail (37), Anwar Nasher Hayel (29) na Yasini Mohamed Shaban (20) mkazi wa Kaloleni.
Kamanda Sabas aliendelea kueleza kwamba, operesheni ya kuwatafuta watuhumiwa wengine wa matukio hayo inaendelea nchi nzima.
“Tunayo majina ya watuhumiwa kadhaa ambao wametoweka Arusha na kwenda kujificha maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Mtuhumiwa mmoja wapo anayetafutwa sana na polisi kuhusiana na matukio haya ni Yahaya Hassan Hella (Sensea) Mrangi ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Chemchem wilayani Kondoa,” alisema Kamanda Sabas.
Alieleza kwamba, mtuhumiwa huyo ndiye kinara wa matukio ya milipuko ya mabomu na tindikali jijini Arusha kwa kushirikiana na watuhumiwa wengine waliokamatwa huku wengine wakiendelea kutafutwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni