Kurasa

Ijumaa, 22 Agosti 2014

MBUNGE WA CCM AJIUNGA UKAWA

Dodoma.Jana ilikuwa kama sinema pale viongozi wa Kamati Namba Moja ya Bunge Maalumu walipojikuta wakibishana na mjumbe wao mbele ya waandishi wa habari, huku siri za mambo ya ndani ya vikao zikianikwa hadharani.
Kamati hiyo inaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu na makamu wake ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, huku ikiwa imesheheni vigogo wengine wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Viongozi wengine katika kamati hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uhusiano na Uratibu), William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
Wamo pia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.
Jana asubuhi, Mwalimu na Profesa Mbarawa walifika mbele ya waandishi wa habari katika Hoteli ya St Gasper wakiwa wameambatana na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy.
Lengo la mwenyekiti na makamu wake lilikuwa ni kumbana Keissy ili akanushe taarifa aliyoitoa juzi kwenye moja ya televisheni kwamba kamati hiyo inaongoza kwa kuvunja kanuni hasa katika suala la akidi ya vikao kutotimia.
Sinema ilivyoanza
Walipofika mbele ya waandishi wa habari, Keissy alipewa fursa ili akanushe taarifa yake, lakini alibadili mada na kuanza kuzungumzia masuala ya muundo wa Serikali na Bunge, huku akisema yeye ni muumini wa serikali tatu na siyo mambo ya serikali mbili zinazopendekezwa na wengi kutoka katika chama chake.
Kauli hiyo iliwashtua Mwalimu na Profesa Mbarawa ambao walianza kumkatisha ili asiendelee.
“Keissy sikukuitia mambo hayo, huu ni mkutano wangu, naomba ukanushe nilichokuitia, hayo utazungumza baadaye tafadhali sana,” alisema Mwalimu.
Wakati huo Profesa Mbarawa na waandishi wa habari waliokuwapo walivunjika mbavu kwa vicheko, huku yeye akiendelea kusisitiza kwamba ni muumini wa Tanganyika.
Wakati akisema hayo, Profesa Mbarawa naye aliingilia kati na kumtaka Keissy kueleza kilichompeleka hapo huku akimtaka aache kelele za kupotosha wananchi kwa kuwa anachosema siyo kweli.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni