Kurasa

Ijumaa, 22 Agosti 2014

CHADEMA WATUNGA WIMBO MAALUM KWAJILI YA MAANDAMANO YA UKAWA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetunga wimbo maalumu kwa ajili ya maandamano yaliyopangwa na chama hicho na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ili kushinikiza Bunge Maalumu la Katiba ambalo linaendelea Mjini Dodoma, lisitishe vikao vyake hadi kuwepo maridhiano.
Wimbo huo ambao ni mahususi kwa ajili ya maandamano ambayo haifahamiki yatafanyika lini, umepangwa kusambazwa kwa wananchi nchi nzima ukifahamika kama mchakamchaka wa katiba.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, Bw. John Mnyika, alisema wimbo huo utaimbwa na wananchi pamoja na wanachama wa vyama vinavyounda UKAWA na kuuimba mbele ya waandishi wa habari.
"Msimamo wa kuandamana nchi nzima uko palepale, tarehe rasmi ya maandamano itatangazwa baadaye...kutungwa kwa wimbo huu ni maandalizi ya awali tukisubiri matokeo ya mazungumzo ambayo yanaendelea nyuma ya pazia.
"Kama hakutakuwa na maridhiano katika mazungumzo hayo, tutaingia rasmi barabarani ili kufanya maandamano...lengo letu ni kutaka maridhiano au mchakato huu usitishwe,"alisema.
Aliongeza kuwa, Kamati Kuu ya CCM kupitia Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya Kikwete, amekosea kutoa uamuzi wa kubariki mchakato huo uendelee badala ya kuusitisha.
Alisema CCM kimedhihirisha msemo wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwa;"Bila CCM thabiti nchi inalegalega", hivyo nchi imeanza kulegalega kutokana na udhaifu wao.
"Kimsingi mchakato huu unapaswa kusimama ili kupisha maridhiano kwanza, kuendelea kwake ni matumizi mabaya ya fedha za Watanzania...sisi tunataka Bunge lisitishwe,"alisema.
Bw. Mnyika alisema ni vyema Rais Kikwete ajitokeze hadharani kuzungumza na wananchi kama alivyo ahidi awali kuwa kama majadiliano yaliyokuwa yakiendelea yakikwama, angeingilia kati ili suluhu iweze kupatikana.
Aliongeza kuwa, CCM kimefuata masilahi yao katika mchakato huo na kuyapuuza mapendekezo ya wananchi hivyo kusababisha nchi ilegelege kutokana na uongozi uliolegalega.
Aliitaka Serikali ya chama tawala, kulinusuru Taifa katika mchakato huo kwa kutafuta maridhiano au kulisitisha Bunge hilo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni