Kurasa

Jumatatu, 7 Julai 2014

UTAFITI NI MUHIMU KATIKA BIASHARA

WATU wengi hufikiri kwamba mtaji ni kigezo pekee cha kuanzisha biashara na kutoona umuhimu wa kufanya utafiti.
Kutokana na hali hiyo, hujikuta biashara zao zikishindwa kuhimili ushindani kwa kuanguka au kukosa wateja.
Unapozungumzia utafiti, watu huchukulia ni masuala makubwa kama ya kisayansi jambo ambalo si kweli.
Utafiti wa kibiashara ni utafiti unaohusu mambo madogo madogo yanayoweza kuathiri au kutoathiri biashara yako.
Ni vizuri ukayafahamu mambo hayo kabla na kujipanga namna ya kukabiliana nayo.
Utafiti ni suala la kulipa kipaumbele kabla ya kuanza biashara ili kumsaidia mfanyabiashara kuzifahamu changamoto za biashara husika anayoenda kuifanya.
Yapo maeneo muhimu ambayo mfanyabiashara anatakiwa kuyafanyia utafiti kabla ya kuanza biashara ambayo ni wateja, utafiti wa bei, washindani, mabadiliko ya tabia ya nchi, magonjwa na hali ya siasa.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Alpha Associate Ltd, inayojishughulisha na masuala ya ushauri kwa wafanyabiashara jijini Arusha, Alphonce Massaga, anasema ni vema mfanyabiashara akafanya utafiti wa wateja anaowategemea kununua bidhaa zake.
Mshauri huyo anagusia suala la utafiti iwapo bidhaa hiyo inakubalika katika jamii husika.
Pia kutazama mila na desturi za eneo husika iwapo zinaruhusu kuwepo kwa biashara husika.
Utafiti wa bei unaofanyika kabla ya kupanga bei ya bidhaa au huduma husika ili kuangalia kama bei hiyo itakubalika, pia unakwenda sambamba na utafiti wa hali ya uchumi wa watu wa eneo husika kwani ukishajua hali zao za kiuchumi ni rahisi kupanga bei inayoshabihiana na kipato cha watu wanaoishi karibu na biashara yako.
Kwa mtazamo wangu ni muhimu kujifunza mbinu wanazotumia wapinzani wako katika biashara. Hapa unapaswa kuangalia bei zao na ubora wa bidhaa ili kujua namna utakavyoshindana nao bila kuanguka kibiashara.
Suala la mbinu za kibiashara na siri zilizoko ndani ya biashara husika unayotaka kuanzisha unaweza ukajifunza kwa watu wanaofanya biashara kama yako walioko maeneo ya mbali.
Ukifanya hayo kwa wale walioko karibu wanaweza wasikupe ushirikiano kwa kuhofia kupitwa.
Pia utafiti wa maeneo ni muhimu kwani unamsaidia mfanyabiashara kugundua fursa zilizopo katika eneo husika ikiwemo mahitaji ya jamii kama chakula, mavazi, malazi, huduma za usafiri na afya ambazo humsaidia mjasiriamali kujua ni biashara gani aanzishe itakayompatia faida.
Pia inamsaidia mfanyabiashara kujua mila na desturi za jamii husika.
Mfano unataka kuanzisha biashara ya suti maeneo ya jamii ya Wamasai ambao wengi wao huvaa migorore (mashuka ya kimasai na vikoi), ni wazi kuwa hutopata wateja na biashara yako haitakuwa endelevu. Hivyo ni vema utafiti wa maeneo ukazingatiwa.
Vilevile katika biashara utafiti juu ya mabadiliko ya tabia ya nchi ni muhimu sana, hasa kwa wale wanaofanya biashara ya mazao ya kilimo, linapokuja suala la ukame linaathiri sana biashara hiyo.
Utafiti huo utamsaidia mfanyabiashara kujua taarifa muhimu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa au kutokana na utafiti alioufanya mwenyewe.
Massaga anasema unakuta mkulima alitarajia kulima hekari 50 ili apate faida, linapokuja suala la mabadiliko ya hali ya hewa linamuathiri kwa kiasi kikubwa pamoja na kupungua kwa kiwango cha uzalishaji, kwa hili wakulima wanaweza kulijua mapema wakifanya utafiti.
Ili kuwa na biashara endelevu inayohimili ushindani na yenye mafanikio, utafiti ni jambo la msingi sana la kuzingatia kabla ya kuanza biashara na baada ya kuanza biashara.
Mtanzania

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni