Kurasa

Jumanne, 24 Juni 2014

TATIZO LA AJIRA NCHINI MTAJI KWA WANASIASA

SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu tatizo la ajira nchini, huku wanasiasa waliozungumzia tatizo hilo kuwa ni bomu, wakitakiwa kutoa ushauri wa namna ya kulitegua au kupunguza athari zake kama likilipuka.
Mbali na ushauri huo, Serikali pia imewataka wanasiasa wanaotumia tatizo hilo kisiasa, kuonesha mfano wa kusaidia vijana katika majimbo yao kwanza, badala ya kusubiri siku wakipewa nchi.
Mawaziri wanne walitumia muda wao jana kujibu hoja hiyo, ambayo ni hoja lulu kisiasa, kutokana na hali halisi kuwa sehemu kubwa ya Watanzania ni vijana, hivyo inatazamwa na wanasiasa wengi kuwa ndio watakuwa sehemu kubwa ya wapiga kura.
Kutokana na umuhimu wa ajira katika siasa za leo, Naibu Spika, Job Ndugai hivi karibuni alisema Mtanzania mwenye nia ya kugombea urais mwaka 2015, ili aeleweke kwa wananchi, ni lazima aeleze mikakati ya kuwasaidia vijana kupata ajira.
“Ajira ni tatizo kubwa na lazima lishughulikiwe. Kuna vijana hawaendi shule, lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne, cha sita na vyuo vikuu.
"Nazungumza kutoka moyoni kabisa. Hizi ni dakika za mwisho za Serikali ya Awamu ya Nne, wale wanaojipanga kwa Awamu ya Tano kama hawataongelea ajira, basi waandike wameumia,”alisema Ndugai.
Alianza Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, ambaye alikiri kuwa ajira ni tatizo, lakini akafafanua kuwa si la Tanzania tu, bali pia ni tatizo la kimataifa.
Alisema katika utafiti uliofanyika mwaka 2012, ilionekana ajira ya muda mrefu, inayompa mwajiriwa hifadhi kuwa imeongezeka kwa asilimia 13.5. Ongezeko hilo limetolewa katika sekta ya umma, ambayo imetoa asilimia 35.8 ya ajira huku sekta binafsi ikitoa asilimia 64.2 ya ajira.
Kutokana na mchango mkubwa wa sekta binafsi katika ajira, Kabaka alisema Serikali imekuwa ikiweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, ikiwemo ujenzi wa barabara, kuboresha upatikanaji wa nishati ya umeme na mawasiliano.
Alisema wakati wanasiasa wanasema Tanzania kuna tatizo kubwa la ajira, ambalo kitakwimu ni asilimia 11.7, nchini Afrika Kusini ni asilimia 24.9.
“Sasa kabla ya kusema ukipewa nchi utatoa ajira, tuoneshe kwanza katika jimbo lako. Umefanyaje kuongeza ajira katika sekta isiyo rasmi…msidanganye wananchi na kuwachonganisha na Serikali,”alisema.
Kuhusu fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo, Serikali imezungumza na Chama cha Waajiri (ATE) ili watoe fursa hizo kwa wanafunzi wanaotoka katika vyuo mbalimbali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, aliamua kuonesha mfano kwa kuanza kutoa ushauri.
Alitoa hatua kumi, alizotaka waajiriwa watarajiwa walio katika soko ambao hawajapata ajira na walio vyuoni na wanaojiandaa kujiunga na vyuo mbalimbali, ili wapate ajira.
Kwanza aliwataka wanafunzi wanaojiunga na vyuo, kama wanataka kuajiriwa, wachukue fani za sayansi, teknolojia na uhandisi.
Pili, aliwataka wanaosomea uhandisi na sayansi, wachanganye fani hiyo na fani ya usimamizi wa biashara.
Tatu, aliwataka wanaochukua fani za sanaa, pia kuchukua fani za usimamizi, kwa maana ya Shahada ya Uzamili ya Usimamizi (MBA).
Profesa Mwandosya pia aliwataka waajiriwa watarajiwa, wasidharau lugha za Kiswahili na Kiingereza ;na wazizungumze kwa ufasaha, lakini akawataka pia kuchukua lugha moja katika ya Kifaransa, Kihispania, Kireno na Kichina.
Hatua nyingine waliyoshauriwa kuchukua ni kutoogopa kushindana katika soka la nje, ikiwemo soko la Afrika Mashariki, Afrika na sehemu nyingine duniani. Kwa mujibu wa Profesa Mwandosya, katika soko hilo la ajira kuna Wakenya, Warwanda na Waganda.
Aliwataka wanafunzi vyuoni kuanza kujijengea kichwani dhana ya kujiajiri, kwa kuwa ni jambo zuri ili wasingoje kupata ajira za Serikali.
Wasomi hao pia walitakiwa waache kuchagua kazi wala ngazi ya kuanzia kazi, kwa kuwa hata aliyesomea uhandisi akianzia kazi ya fundi mchundo, atapanda haraka. Pia, aliwataka wajiamini, wawe wabunifu na kujiunga katika vikundi ili wawezeshwe.
HABARI LEO

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni