Kurasa

Jumapili, 1 Juni 2014

MTOTO AMUUA MDOGO WAKE KWA BASTORA

Payson Ariz, mtoto wa kiume wa miaka mitatu amemuua mdogo wake wa kiume mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu kwa kumpiga risasi.
Mtoto huyo alimuua mwenzake baada ya kukuta mfuko wa silaha hiyo katika chumba cha jirani na kwenda nao katika chumba kingine kabla ya kumfyatulia risasi mdogo wake.
Mkuu wa Polisi wa Jimbo la Arizona, Don Engler alisema uchunguzi wa idara yake kuhusu tukio hilo lililotokea Jumanne wiki hii, utachukua wiki moja, huku matokeo yakipelekwa katika ofisi ya mwanasheria iwapo kukiwa na mashtaka yoyote.
“Kitakachoangaliwa zaidi ni kuhusu utunzaji silaha kwa usalama zaidi na namna watoto hao walivyoweza kuibeba silaha hiyo ikilinganishwa na uzito wake, sisi tunaendelea na uchunguzi wetu,” Don aliliambia Shirika la Habari la Associated Press.
Alisema kuwa ni mapema kueleza mapendekezo ya idara yake, lakini anapisha uchunguzi ufanye kazi yake.
Wavulana hao pamoja na mama yao walikuwa wamemtembelea jirani yao mwenye umri wa miaka 78 katika jengo analoishi, kabla ya mlio wa risasi kusikika kwenye chumba cha kulala cha mzee huyo. Mtoto aliyempiga mwenzake risasi alikutwa akiwa ameshikilia bastola hiyo, huku akiendelea kushangaa kilichotokea.
MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni