Kurasa

Jumapili, 15 Juni 2014

KESI YA KUPINGA MCHAKATO WA KATIBA MPYA KUTOKANA NA MATUMIZI YA MABILIONI YA FEDHA ILIIYOFUNGULIWA NA WAZALENDO WAWILI KUHAMIA DAR

Moshi. Kesi ya kikatiba iliyofunguliwa Mahakama Kuu Moshi na wananchi wawili wakitaka kusimamishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya likiwamo Bunge la Maalumu la Katiba, sasa imehamishiwa Jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo imehamishiwa Masjala Kuu ya Mahakama Kuu wakati wananchi hao wakijiandaa kuwasilisha ombi chini ya hati ya dharura, wakitaka Bunge Maalumu la Katiba lizuiwe kuendelea na vikao vyake mwezi Agosti. Walalamikaji katika kesi hiyo, iliyofunguliwa mwezi uliopita na awali kupangwa kutajwa Agosti 28 kabla ya kubatilishwa, wanatetewa na wakili Jimmy Obed kutoka Kampuni ya Jimmy & Company Advocates ya Jijini Dar.
Uamuzi wa kulihamisha jalada la kesi hiyo, umetolewa na Jaji Amaisario Munisi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi na kuifuta pia tarehe ambayo shauri hilo lilipangwa kutajwa Agosti.
Jaji Munisi alisema anatambua kuwa shauri hilo ni la kikatiba linalohitaji kusikilizwa na Majaji watatu, hivyo analihamishia Masjala Kuu Jijini Dar kwa ajili ya taratibu hizo na wadai wajulishwe juu ya uamuzi huo.
Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu Serikali (AG) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.
“Nina maelekezo kutoka kwa wateja wangu kuwa kabla ya siku hiyo ya kusikilizwa kwa kesi niwasilishe maombi ya hati ya dharura kusimamisha vikao vya Bunge la Katiba,”alisema.
Katika kesi hiyo, wananchi hao wanadai kuwa licha ya mchakato mzima wa Katiba kuwa batili, unakiuka Sheria za kimataifa na ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi wa Tanzania.
Wananchi hao wamefungua kesi wakati taarifa zikieleza kuwa kwa siku 67 Bunge la Katiba lilipokutana, lilitumia Sh27 bilioni na pia linatarajia kutumia Sh20 bilioni litakapokutana kwa siku 60 kuanzia Agosti 5.
Mbali na matumizi hayo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake Jaji Joseph Sinde Warioba iliyokusanya maoni inaelezwa kutumia Sh69 bilioni za walipa kodi wa Tanzania.
Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa Mahakama Kuu, moja kati ya maombi wanayoomba, ni mahakama itamke sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012 ilikiuka Katiba ya mwaka 1977.
Pia wananchi hao , wanaiomba mahakama itamke kuwa Bunge Maalumu la Katiba ni batili.
Wananchi hao wanadai kuwa mchakato huo ni batili kisheria kwa vile miongoni mwa mambo yaliyomo katika rasimu ya katiba yanalenga kuzungumzia kero zilizomo kwenye Muungano.
MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni