Kurasa

Jumapili, 15 Juni 2014

HAZINA KUTUMIA MABILIONI YA PESA KWAAJILI YA POSHO

Dodoma. Wakati Serikali ikihaha kusaka fedha za kugharimia miradi ya maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha, kumekuwa na shaka kuhusu uhalisia wa hesabu za matumizi zilizotengwa kwa ajili ya Ofisi ya Hazina.
Ofisi hiyo chini ya Fungu 21 imeomba kuidhinishiwa kiasi cha Sh790,325,216,000 kwa ajili ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa kupitia katika idara zake kati ya hizo zaidi ya Sh50 bilioni zikiwa ni kwa ajili ya safari na posho mbalimbali.
Itakumbukwa kuwa tangu kumalizika kwa uwasilishaji wa bajeti za kisekta kupitia wizara za Serikali, Kamati ya Bunge ya Bajeti imekuwa katika mashauriano na Serikali, kusaka fedha kwa ajili ya utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo ilionekana kuwa ni muhimu.
Katika mashauriano hayo, Serikali na kamati zilikubaliana kukata asilimia nane ya fedha za matumizi mengine katika kila wizara na kuchukua kiasi cha Sh2 bilioni kutoka Hazina maalumu ya Serikali ili kupata Sh225.281 bilioni kwa ajili ya maeneo yaliyokuwa na upungufu.
Wakati hayo yakiendelea mabilioni ya fedha yametengwa kwa ajili ya kazi za idara zilizopo chini ya Hazina ambazo kimsingi zinapaswa kufanywa na watumishi wa Serikali katika kazi zao za kawaida bila kupewa malipo ya ziada.
Ufafanuzi wa matumizi ya fedha uliotolewa kwenye Randama za Hazina unaonyesha kuwa baadhi ya fedha zimetengwa kwa jumla tu, pasipo kuonyesha uhalisia wa matumizi yake.
Miongoni mwa maeneo yaliyotengewa kiasi kikubwa cha fedha ni kile kinachoitwa malipo ya tuzo kwa watumishi, vifaa vya nyumbani kwa baadhi ya wakurugenzi na wakuu wa idara, posho za vikao maalumu na malipo kwa ajili ya kazi ambazo kimsingi ni wajibu wa idara husika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luhaga Mpina, alisema Serikali haijapunguza matumizi mengineyo katika bajeti zake za mwaka wa fedha 2014/2015 kama ilivyoahidi katika bajeti iliyopita.
Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa (CCM), alisema Serikali iliahidi kupunguza matumizi mengineyo (OC) kwa kiasi cha Sh283 bilioni katika mwaka wa fedha 2013/2014, lakini hakuna ushahidi kwamba imetekelezwa.
“Ahadi hiyo ilitolewa kwa maandishi na Waziri wa Fedha, lakini hadi mwaka mwaka huu wa fedha unaelekea mwisho hakuna mchanganuo wowote unaoonyesha kupunguzwa kwa matumizi hayo,” alisema Mpina na kuongeza: “Bunge lilihakikishiwa kuwa kuhamishwa kwa fedha hizi na kupelekwa katika miradi ya maendeleo hakutaathiri utendaji wa Serikali. Lakini cha kushangaza, bajeti iliyowasilishwa matumizi mengineyo (OC) yameongezeka.”
Alisema wakati wa uwasilishaji wa maoni ya kamati yake kuhusu Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2014/2015, kamati ilihoji kwa nini kwa kipindi kirefu Serikali imeendelea kutetea matumizi ya aina hii kuwa ni muhimu, lakini Serikali haijawahi kuleta mchanganuo wa matumizi hayo (matrix) ili kuthibitisha umuhimu unaosisitizwa?
MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni