Kurasa

Ijumaa, 23 Mei 2014

WATAALAMU WAINGILIA DHAHABU YA WANANCHI LOLIONDO KWA BABU.

MKUU wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, amesema kuwa wataalamu wa madini wanaendelea na utafiti kubaini endapo madini yanayoendelea kuchimbwa na wananchi kwenye maeneo ya milima na Mtoni kwenye Kijiji cha Samunge ni dhahabu kweli.
Aidha amekanusha taarifa zilizozagaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa kuna ongezeko kubwa la watu kwenye kijiji hicho toka maeneo mbalimbali ya nchi tokea kubainika kuwepo kwa dhahabu hiyo katikati ya Machi mwaka huu, akisema kuwa wageni hawazidi asilimia 5.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, alisema kuwa wataalamu hao kutoka ofisi ya madini Kanda ya Kaskazini wanatazamiwa kumpatia matokeo ya utafiti huo wakati wowote.
Wawa Lali alisema kuwa hakuna madini yanayookotwa juu ardhi bali yanachimbwa, huku akionya kuwa huenda upotoshaji huo unafanywa ili kunufaisha baadhi ya watu ikiwemo kijiji hicho ambacho hutoza sh 10,000 kwa kila mtu anayeingia.
Hata hivyo, alisema kuwa baada ya matokeo ya wataalamu wa madini kutolewa na ikibainika ni madini ya aina gani yanayopatikana Samunge, serikali itatoa muongozo juu ya namna ya kuyachimba ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza endapo watu wataachwa kuchimba holela kama ilivyo sasa.
Alifafanua kuwa hakuna watu 4,000 kwenye Kijiji cha Samunge kama inavyoelezwa, kwani kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika kijijini hapo, watu wanaochimba madini hayo ni kati ya 500 hadi 600 na kati yao wenyeji wa kijiji hicho ni asilimia 80.
Alisema kuwa wengine asilimia 10 wanatoka ndani ya Kata ya Samunge na tano wanatoka wilayani Ngorongoro, huku asilimia tano tu ndio wanaotoka nje ya Kata ya Samunge.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni