Kurasa

Ijumaa, 23 Mei 2014

MGANGA AMNYONGA NA KUMKATA SEHEMU ZA SIRI MTOTO WA MIAKA NANE.

MTOTO Fausta Geofrey (8), mkazi wa wilayani Muleba, ameuawa kikatili kwa imani za kishirikina na mganga wa kienyeji kwa kunyongwa na kisha kukatwakatwa mapanga na kuondolewa baadhi ya viungo vyake, zikiwemo sehemu za siri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Mei 21 mwaka huu, saa 1:30 asubuhi katika Kijiji Cha Bisole, Kata ya Muhutwe, Wilaya ya Muleba.
Alisema mtoto huyo ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kitunga, akiwa na wenzake wakielekea shuleni, walipofika eneo la mganga huyo wa kienyeji, Mujingwa John (20 alimkamata na kumpeleka ndani kwake kisha kumnyonga hadi kufa.
Kamanda Mayunga alisema mganga huyo baada ya kumkaba shingo mtoto huyo, alimkata mkono wa kushoto, masikio, sehemu za siri na sehemu nyingine za mwili.
Alisema viungo hivyo alivibanika ili vikauke na baadae atengeneze dawa kwa matumizi mengine.
Kamanda Mayunga alisema baada ya kutoa viungo hivyo, sehemu ya mwili iliyobaki alichimba kaburi chini ya kitanda chake na kuvizika kisha kuweka nyasi juu yake.
Alisema siku ya tukio wazazi wa mtoto huyo walipatwa na wasiwasi baada ya mtoto wao kutorudi nyumbani, hivyo walitoa taarifa kituo cha polisi Muleba.
Kamanda Mayunga alisema baada ya taarifa kufika kituo cha polisi walishirikiana na wazazi kumtafuta wakapata habari za mtoto huyo kuchukuliwa na mganga huyo na alipokwenda kuhojiwa alikana, lakini alipobanwa alikiri na kuwaeleza anaye lakini ameshakufa.
Alisema alifanya hivyo kwa sababu ya kukosa fedha za kujikimu kimaisha.
“Nilikuwa nataka kuwa tajiri ndiyo maana nilijiingiza kwenye uganga,” alisema mtuhumiwa huyo ambaye bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi.
TANZANIA DAIMA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni