Kurasa

Jumatatu, 12 Mei 2014

WAHANDISI WAONYWA KUACHA KUTUMIWA NA WANASIASA.

Dar es Salaam. Wahandisi na mafundi nchini wameonywa kutokubali kutumiwa na wanasiasa badala yake wafanye kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia taaluma zao.
Hayo yalisemwa jana na Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzani(IET), Dk. Malima Bundara wakati akitoa mapendekezo yanayohusu mafuriko nchini na msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Dk Bundara alisema wahandisi na mafundi hao wamekuwa wakijisahau na wakati mwingine kutumiwa na wanasiasa na kuwataka kutambua nafasi zao kwa sababu wao ni watendaji na wanatumia utaalamu zaidi.
Alisema si sawa kwa mtaalamu kufanya shughuli zake kisiasa na kuwashauri kuacha tabia ya kukubaliana na wanasiasa kujenga majengo kwenye mikondo ya asili ya maji na fukwe za bahari huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kwani kunazuia maji kuingia baharini.
“Wahandisi na mafundi mnatakiwa mfanye kazi kwa kuzingatia taaluma zenu, mtakapowasikiliza wanasiasa mtakiuka sheria na kuonekana wenye matatizo kitaalamu,”alisema Dk Bundara.
Akizungumzia wiki ya maadhimisho ya wahandisi yanayotarajiwa kufanyika Septemba 21 hadi 26 mwaka huu, amesema yatahamasisha kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda mazingira.
Alisema wanaoishi mabondeni wajue kuzibwa kwa njia za asili za maji kuna athiri.
Via.MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni