Kurasa

Jumapili, 18 Mei 2014

MASKINI WAFUNGWA KUMBE WANAKULA MIA TANO TU KWA SIKU.

Dodoma.Wakati idadi ya wafungwa ikizidi kuongezeka nchini, Serikali imesema katika mwaka wa fedha 2014/15 itaendelea kumlisha mfungwa mmoja kwa Sh500 kwa siku.
Licha ya kuwa kiwango hicho cha fedha ni kidogo serikali inasema kuwa kama idadi ya wafungwa ikiongezeka, inagawanywa na inawezekana kila mfungwa, kulingana na eneo husika akatumia Sh250 kwa siku.
Hayo yalielezwa juzi jioni na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge kabla ya kuanza upitishwaji wa vifungu vya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2014/15.
Wakati Chikawe akieleza hayo, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka wa fedha ulioisha mwaka 2013, inaeleza kuwa nchini kuna magereza 122 na yanatoa huduma kwa wafungwa 45,000, wakati uwezo wa magereza hayo ni kuwahudumia wafungwa 22,669.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo chakula cha wafungwa kilitakiwa kutengewa Sh32 bilioni lakini bajeti iliyoidhinishwa ilikuwa Sh8 bilioni ikiwa ni pungufu ya Sh24.4 bilioni.
Katika ufafanuzi wake Chikawe alisema, “Kiwango cha fedha tunachotoa kwa mfungwa na mahabusu kwa siku ni Sh500. Kiwango hiki ni kidogo ikilinganishwa na gharama halisi za maisha,” alisema Chikawe na kuongeza;
“Mwaka jana katika mazungumzo na Kamati ya Kudumu ya Ulinzi na Usalama tulikubaliana kiwango kifike Sh1,500 kwa siku, lakini hali ya bajeti wakati ule haikukidhi matakwa yetu na hivyo hatukupata kiwango hicho.”
Alisema hivi sasa wizara hiyo ipo katika mazungumzo na Hazina ili kuona kama kuna uwezekano wa kupandisha kiwango hicho hadi Sh3,000, kusisitiza kuwa kama kiwango hicho kikishindikana wataomba hata kupewa Sh1,500 kwa siku.
“Kuna wakati mahabusu wanakuwa wengi hivyo kiwango cha Sh500 tunachowatengea kinakuwa chini,” alisema.
Akizungumzia madeni yanayozikabili idara zilizopo chini ya Wizara hiyo, Chikawe alisema, “Jeshi la Magereza lina deni la Sh65 bilioni, Polisi Sh123 bilioni,”
“Pia kuna madeni ya watumishi, likizo na stahiki zao mbalimbali, madeni ya wanaotoa huduma za mafuta na chakula katika idara hizo pamoja na mikopo na riba kwa mashirika mbalimbali kama NSSF.”
Alisema kuwa kila Wizara inapoomba bajeti kubwa kwa ajili ya kukidhi utekelezaji wa mambo mbalimbali haipati fedha kwa wakati jambo ambali limeifanya kulimbikiza madeni.
via:Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni