Kurasa

Jumatatu, 19 Mei 2014

MAANDALIZI UCHAGUZI MALAWI YAMEKAMILIKA,JE MWANAMKE JOICE ATARUDI?

Maandalizi kwa ajili ya uchaguzi Mkuu wa Malawi yamekamilika huku wagombea kumi na mbili wakikabana koo kuwania kiti cha urais wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi huu, kampeni zote zinapaswa kumalizika saa 48 kabla ya muda wa kuanza kupiga kura..na kwahivyo harakati za wagombea na wapiga debe wao kunadi sera na kujitangaza kwa miezi miwili, zilimalizika asubuhi ya jana Jumapili.
Huu ni uchaguzi wa kwanza katika historia ya Malawi wananchi kupiga kura tatu kwa wakati mmoja, zikiwemo za Urais, Wabunge na Madiwani.
Ni mchuano wa kugombea nafasi moja ya Urais, viti 193 vya ubunge na madiwani 462.
Wamalawi milioni saba na nusu wamejiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huu unaoshirikisha vyama 12 vya siasa vikiongozwa na chama tawala Peoples Party - PP cha Rais wa sasa Joyce Banda.
Japokuwa kuna msururu wa vyama vilivyosimamisha wagombea urais, lakini ni wanne tu miongoni mwao wanaoongoza mbio za kwenda ikulu ya Sanjika Palace mjini Blantyre.
Rais Joyce Banda ambaye mashabiki wake wanamuita JB mwanamke shupavu, anawania kubaki Sanjika Palace kwa tiketi ya PP chama ambacho alikianzisha mwaka 2012 baada ya kufukuzwa kutoka DPP.
'Uchaguzi wa hesabu'
Uchaguzi huu unachukuliwa na wengi nchini hapa kama uchaguzi wa hesabu kubwa na wenye mitego mingi hasa kutokana na aina ya wagombea Urais..
Sehemu kubwa ya ahadi kutoka kwa wagombea wote ni ile ya kujenga uchumi imara wa nchi hii, ajira kwa vijana pamoja na suala la kuboresha kilimo na kuwawezesha wakulima wa Tumbaku zao linalotegemewa zaidi kwa uchumi wa Malawi,wapate faida kuliko ilivyo sasa..
Rais Banda anamenyana na wagombea wengine 11........
Jambo la kufurahisha hapa ni kwamba wamalawi wamepata nafasi ya kufanya uchaguzi wa ama kumbakiza Rais Banda au kukirudisha DPP ambacho kilipoteza mamlaka yake baada ya kufariki kwa Bingu wa Mutharika na sasa wampe ikulu mdogo wake Profesa Peter Mutharika.
Lakini pia wananchi hawa wana uamuzi mwingine wa kusema hawataki tena kurudia rudia wanasiasa na vyama vile vile..na hivyo wampatie uongozi wa nchi mchungaji Dr Lazarus Chakwera ambaye wakati wa kufunga kampeni zake hapa mjini Lilongwe alitangaza mali zake anazomiliki.
Yeye anasimama kwa tiketi ya chama kikongwe na cha ukombozi wa Malawi- MCP kilichokuwa kikiongozwa na marehemu Dr Hastings Kamuzu Banda…chama hiki kimepotea madarakani kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Ama pia waamue kumpatia urais kiongozi kijana mwenye umri wa miaka 37 Atupele Muluzi. Huyu ni mtoto wa Rais wa pili wa Malawi Bakili Muluzi. Kwa namna yake amekuwa kivutio kwa vijana wenzake wengi nchini hapa.
'Wafungwa wagoma kupiga kura'
Baadhi ya mambo yanayowakera wananchi wa Malawi ni jinamizi la ufisadi, gharama ya juu ya maisha na mengineyo........
Sehemu kubwa ya vyama vingi hapa Malawi ni vipya kabisa kikiwemo chama tawala cha Rais Banda na United Independece UIP ambacho kinaongozwa na mgombea urais wake mwana mama mwenye asili ya kiasia Abusa Hellen Singh na mgombea mwenza wake pia ni mwanamke Madam Chrissy Tembo.
Wakati hayo yakiendelea baadhi ya wafungwa katika magereza wamegoma kuwa hawatakubali kupiga kura hapo kesho kwa kuwa tu wagombea urais hawakupita magerezani kunadi sera zao.
Ikumbukwe kwamba wafungwa nchini hapa wanaruhusiwa kupiga kura.
Baadhi yao wamehoji itakuaje wapige kura ya Rais peke yake ilhali wao wana makwao na wangependa kupiga kura za wabunge na madiwani wao. Lakini hilo linapata kikwazo cha kisheria kwani wafungwa wameruhusiwa kupiga kura ya Rais tu.
Vyovyote itakavyokuwa uamuzi ni wa wamalawi watakaojitosa kupiga kura katika zaidi ya vituo 11,000 nchini kote..ambapo waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wale wa kimataifa wametapakaa kila mahali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni