Kurasa

Jumamosi, 17 Mei 2014

KWA HILI WAZANZIBARI NI SAWA KUTOKA NJE YA BINGE.

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imesema kauli ya kuudhi iliyotolewa bungeni juzi jioni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Frederick Werema imekuzwa na kuyumba kwa Kiti cha Spika.
Imesema ndani ya Bunge hilo kuna viongozi wenye uzoefu kutokana na kuwepo bungeni kwa muda mrefu, hivyo wanatakiwa kutumia uzoefu wao kuliongoza vyema bunge.
Juzi Werema alitoa kauli ya kuudhi kabla baadaye kuomba radhi, akimtaka Mbunge wa kutoka jimbo la Mkanyageni Zanzibar (CUF), Habibu Mnyaa akaulize swali lake Visiwani na kusababisha wabunge kutoka Zanzibar kususa na kutoka nje sambamba na wabunge wote wa upinzani isipokuwa John Cheyo (UDP).
Uamuzi wa kutoka ulitokana na Spika wa Bunge, Anne Makinda kukataa mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Ole (CUF), Rajabu Mbarouk Mohamed, aliyehoji uhalali wa kauli ya Mwanasheria Mkuu kutolewa bungeni, akisisitiza kuwa ni ya kibaguzi.
Akizungumza bungeni jana kwa niaba ya Kambi ya Upinzani Bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu, huku akinukuu Biblia na Quran, Mbatia alisema, “Kila mtu akitoa kauli ana haki ya kujibiwa, lakini viongozi wengine wana uzoefu na wanatakiwa kutumia katika uongozi.”
“Hata kama kiti kina mapenzi na upande fulani humu ndani ya bunge kinatakiwa kutenda haki bila kuegemea upande wowote,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema kambi hiyo itaendelea kuamini katika mfumo wa Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika na kwamba Wazanzibari waliopo ndani ya Bunge hilo wana haki ya kujibiwa maswali kwa mujibu wa sheria na Katiba.
“Tumeridhia ombi la Werema la kuomba radhi na kauli aliyoitoa iwe changamoto kwetu sisi wengine. Hatutakiwi kuonyesha siasa za kibabe,” alisema Mbatia.
Mbatia alisisitiza kuwa wabunge wote wa upinzani wataendelea kuingia katika vikao vya Bunge kama kawaida, huku Naibu Spika Job Ndugai akiwataka kusahau yote yaliyopita.
Ilivyokuwa
Mnyaa aliuliza swali lake wakati wa kupitisha vifungu vya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/15.
Alisema Wizara ya Katiba na Sheria ni muhimu lakini imekuwa ndiyo ya kwanza kuvunja sheria na haki za binadamu na akataka ufafanuzi.
Via:Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni