Kurasa

Jumatatu, 12 Mei 2014

KWA DENI LA TAIFA SASA KILA MTANZANIA ANADAIWA 470000/-

WAKATI maisha ya watanzania yakizidi kuwa mabaya kila kukicha kutokana na uchumi wa nchi kushuka, ibebainika kwamba deni la Taifa limezidi kupanda kila mwaka hadi kufikia trilion 21.2 mwaka 2013/2014. kupanda kwa deni hilo pia limesababisha mfumko wa bei huku shilingi ya Tanzania ikizidi kushuka kutoka shilingi 800 kwa dola moja ya Marekani mwaka 2005 hadi shilingi 1630 kwa dola moja ya Marekani mwaka 2014.
Ramani ya Tanzania ikiwa imepambwa na rangi ya pendela yake.Matokeo ya Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) yameonesha wazi kuwa deni la Taifa limepanda kwa kasi kubwa hadi kufikia trilion 21.2 mwaka 2013/2014. Mwaka 2011/2012 deni la Taifa lilikuwa trilion 16.98. Deni hili la sasa la Trilion 21.2 kwa taarifa ya CAG kama likigawiwa kwa watanzania takribani milion 45, kila Mtanzania wake kwa waume, watoto kwa wazee na vijana watalazimika kulipa tshs 471,111/- ili kumaliza deni hilo.
Hii ni sawa na kusema kuwa kila mtanzania anadaiwa kiwango hicho cha pesa.Kwa namna hiyo,watu wote lazima watayarishwe kulikabili kulilipa deni la Taifa. Ni lazima sote tujitayarishe kuumia sana, hakuna asiyejua machangu ya kulipa deni linalokuzidi umri, uwezo, ni dhahiri deni la Taifa limefikia kiwango cha kutisha na huko tunakoelekea, itabidi serikali ama isimamishe utoaji wa huduma za jamii ili kulipa deni ama kuuza sehemu za tunu zake za Taifa ili deni lilipwe, hivyo ndivyo watanzania watakavyo umia kulipa deni hili.
Ni lazima wananchi waelimishwe kwa namna hiyo kuwa watawajibika kulipa deni hili kwa gharama kubwa, watayarishwe kulikabili deni ambalo limesababishwa na udhaifu wa viongozi wenye matumizi mabaya ya pesa ambazo ni kodi za watu walao kwa jasho lao. Watanzania leo tunakabiliwa na deni hili ambalo limeendelea kukua kwa haraka zaidi kuliko hapo zamani.
Watanzania wanajiuliza maswali mengi ambayo hakuna hata mmoja anayeweza kuyajibu, kama thamani ya maisha wanayoishi leo inaenda sambamba na kiwango cha uwekezeji kilichowekezwa na Taifa kulingana na kiwango hiki kikubwa kupindukia cha pesa zilizokopwa,. Pesa hizo zimetumika kufanya miradi gani ya maendeleo ambayo kama Taifa kwa vyanzo vyetu vya ndani vya mapato tusingeweza kuifanya?. Bila kusita na tukiacha sababu zilizotajwa na CAG, ni lazima Viongozi serikalini wakiri kufanya makosa kuwa ni matumizi mabaya ya pesa, kutokuwepo kwa nidhamu ya matumizi ya pesa za umma ndio chanzo cha kupanda kwa deni la Taifa, ipo mifano mingi ambayo iko wazi inayoonesha kukosekana kwa nidhamu ya matumizi ya pesa za umma.
Nidhamu mbaya ya matumizi ya pesa za umma ndizo zimetufikisha hapa, hivi leo wananchi wanaotawaliwa katika awamu hii ama ijayo wanakabiliwa na deni ambalo linakua kwa haraka kuliko hapo zamani, deni ambalo hata likigawiwa kwa kila mtanzania bado halilipiki kabisa kwa mwananchi wa kawaida aliyejeruhiwa na maisha.
Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Anne Makinda.Japo wapo viongozi wengi wanaojisifu nchi kukopa na wanasema ina sifa za kukopesheka, viongozi hawa wanapaswa kutambua kuwa hiyo sio sifa njema sana kwa Taifa, viongozi hawa wanapaswa kutambua kuwa kama kweli tunakopa tufanye hivyo kwa maslahi ya umma na kamwe mikopo isije kuachwa ikaelemea Taifa na wananchi wakabaki wanataabika viongozi hawa wawe na ujasiri wa kusema wakati wakiwa wenye maisha yasiyo ya anasa na wapole, na kwa namna hiyo wawe ni mfano kwa umma katika matendo halisi. Na hapo ndipo tuta waamini kweli wanakopa kwa maslahi ya wananchi watu walao kwa jasho lao.
Ningeshauri ujenzi mpya wa rasilimali ili kama taifa tupanue zaidi uzalishaji mali za nchi yetu! Hivi sasa nchi imeingia katika deni kubwa kupindukia wakati hatuna hata kiwanda kimoja kama taifa cha kujivunia, kama tungekopa na kuweka mkazo katika viwanda na shughuli za migodi ili kuzalisha mali na kwa ajili ya kuendeleza mbele zaidi uchumi wa taifa, hili tungeliunga mkono.
Kama tungekopa na kuwekeza katika kupeleka mbele juhudi kazi ya uchunguzi wa kisayansi katika pande zote kama migodini, uchunguzi wa mali asili chini ya ardhi, uchunguzi wa kuchimbua vizuri mali hizo sisi wenyewe kama watanzania, uchunguzi wa usafishaji kamili wa mawe ya madini na kadhalika, tungekuwa na amani. Kama taifa tulipaswa tuweke mbele zaidi shughuli za migodi kuliko viwanda vya kutengeneza. Kama taifa leo hii tulipaswa kuzidisha uwezo wa processing raw materials and products,.
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete akitafakari jambo.Nchi yetu imejaa madini ya aina zote, lakini tumeshindwa kuzitumia hali zote hizi nzuri tulizonazo katika kuinua uchumi wa taifa, matokeo yake tunaangukia kukopa huku uchumi wa wanaotukopesha ukipaa kwa,rasilimali zetu. Kama taifa leo hii tulipaswa kueneza nguvu za umeme mashambani ili kutimiza kazi ya umwagiliaji maji mashamba na kueneza utumiaji wa mashine na kujenga vijiji vya kilimo kwa namna ya kisasa kabisa.
Katika nchi yetu karibu asilimia 80 ni wakulima hivyo kama taifa ingekuwa ni jambo la maana sana kusitawisha uchumi wa taifa na kufanya bora maisha ya watu kwa kuinua sekta ya kilimo. Chemchemu ya kuinua kwa mfululizo hali ya maisha ya watu wanaoishi kwa jasho lao iko katika kuongezeka kwa utaratibu kwa mapato ya Taifa.
Hali ilivyo sasa, pato la taifa lipo chini sana na pia pato la mwananchi wa kawaida lipo chini ya dola moja. Serikali lazima ijitahidi kwa kila njia kuongeza mapato ya taifa kwa kustawisha kwa haraka sana viwanda, kilimo na matawi yote mengineyo ya uchumi wa taifa, wakati huo huo iangalie sana kuwepo kwa ugawaji ufaao wa mapato ya taifa kwa kufuata kanuni ya kurekebisha vyema mlingano baina ya uwekaji akiba na matumizi na kanuni ya kuinua hali ya maisha ya watu.
By Marco Amasi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni