Kurasa

Jumamosi, 17 Mei 2014

JUMA KASEJA AWA KOCHA.

Kipa wa Yanga, Juma Kaseja amehitimu mafunzo ya awali ya ualimu wa mpira wa miguu na kupata alama ya daraja A katika mafunzo yaliyoanza Mei 5 mwaka huu na kumalizika jana katika Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na gazeti hili katika ukumbi wa Bwalo la Umwema la JWTZ, Mkufunzi wa mafunzo hayo Meja Mstaafu Abdul Mingange alisema Juma Kaseja ni miongoni mwa wanafunzi 34 waliomaliza kozi hiyo huku watatu kati yao wakipata alama ya daraja la A.
Mingange alisema waliopata daraja A ni Kaseja, Emmanuel Majengo na Richard Ngwanda baada ya kufanya vizuri katika mitihani ya darasani na vitendo vya uwanjani.
“Juma Kaseja amepata alama ya daraja A na wengine wawili, huku waliopata daraja B ni 16 na watano walipata daraja C,”alisema Mingange.
Mkufunzi huyo alisema kuwa vitu walivyojifunza kwa siku 10 katika mafunzo hayo ni pamoja na mpira kinadharia na vitendo, sheria 17 za mchezo wa soka na matibabu ya wanamichezo.
“Kila muhitimu tumempatia CD za kufundishia na vitabu vya muongozo wa namna ya kufundisha mchezo wa soka na baada ya miezi sita wanaruhusiwa kuchukua kozi ya pili kujifunza zaidi,”alisema Mingange.
Akizungumzia juu ya kuchukua mafunzo ya kozi ya awali ya ualimu wa soka, Kaseja alisema amekuwa akifanyishwa mazoezi ya soka, lakini hakuwa anaelewa ni kwa nini anafanyishwa mazoezi na faida yake, baada ya kupata mafunzo hayo hivi sasa anaelewa faida yake.
Kaseja alisema kwa sasa anajua mambo mengi ikiwamo kupanga programu za kufundisha mchezo wa soka na sheria za soka ingawa baadhi alikuwa akizifahamu.
“Wenzetu wachezaji wa Ulaya jambo hili siyo geni, tumeshuhudia Ryan Giggs wa Manchester United akicheza soka na kufanya kazi ya ukocha, hili linafaa kuigwa kwani moja ya faida ya kupata mafunzo ya ukocha huku unacheza ni kufahamu mambo mengi ndani ya soka kwani yatakuepusha kufanya makosa yatakayoigharimu timu,”alisema Kaseja.
Kaseja alisema baada ya kuhitimu kozi hiyo ya awali dhamira yake siyo kuacha soka ila ni kuongeza ujuzi na kuwataka wachezaji wenzake kufanya uamuzi wa haraka wa kupata kozi hiyo.
“Sina mpango wa kustaafu soka leo wala kesho eti kwa sababu nimehitimu mafunzo haya ya ualimu wa soka, naongeza ujuzi tu kwani siku za usoni nitaamua niendelee na soka au nifanya mambo mengine nje ya soka,”alisema Kaseja.
Ktk Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni