Kurasa

Alhamisi, 15 Mei 2014

IFAHAMU HISTORIA YA DENGUE,DALILI ZAKE NA KINGA.

DENGUE ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kinachoenezwa na mbu aina ya Aedes.
Ugonjwa huu umesambaa zaidi katika nchi zenye ukanda wa joto na takribani asilimia 40 ya watu wote duniani wanaishi katika nchi zenye ugonjwa huu.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO)zinathibitisha kuwa takribani matukio milioni tano ya ugonjwa huu yanatolewa kila mwaka na hulazwa hospitali kwa kuathirika na dengue kali; na hii imeshatokea katika nchi zipatazo 34 barani Afrika.
Hapa Afrika ugonjwa huu unajulikana kwa kiwango kidogo licha ya kwamba milipuko ya kwanza umetokea mwanzoni mwa karne ya 19; matukio ya kuongezeka kwa ugonjwa huu yalianza mwaka 1980 katika ukanda wa Mashariki mwa Afrika ikiwa ni pamoja na Msumbiji, Somalia, Kenya, Komoro,Djibouti na Tanzania.
Namna unavyoambikizwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo anasema ugonjwa huo huambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kuumwa na mbu jamii ya Aedes.
Mbu huyu anayeishi katika mazingira ya makazi ya binadamu na huuma wakati wa mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo yenye vivuli hususani majira ya asubuhi na jioni kabla jua halijazama.
Akifafanua zaidi anasema mbu huyu anazaliana katika maji yaliyotuama hasa kwenye vyombo vya nyumbani, makinga maji ya paa za nyumba, matairi ya gari, ndoo, makopo ya kuotesha maua, vikombe, vifuu vya nazi, majani mapana yanayohifadhi maji na hivyo kufanya bustani za maua kuwa mahali pazuri pa mazalia ya mbu hao.
Anasema ugonjwa huu haumbukizwi kwa kumhudumia mgonjwa au kugusa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa na pia hutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka japokuwa hadi sasa bado hakujawepo na dawa maalum ya ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa hutibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huo kama vile homa, kupungukiwa maji au damu.
Dalili za ugonjwa
Katika uuguaji wa ugonjwa huu, kuna aina tatu zinaweza kujitokeza moja ikiwa ni homa ya dengue, ambako aina hii huambatana na homa ya ghafla, kuumwa kichwa na maumivu ya viungo na uchovu.
Kwa Tanzania hadi sasa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wameonekana na dalili hizi.
Aina ya pili ni dengue ya damu, ambako hii huambatana na dalili za mgonjwa kutokwa damu kwenye fizi au puani, vilevile kutokwa damu chini ya ngozi na iwapo mgonjwa mwenye dalili hizi ataumia sehemu yoyote ni rahisi kwake kupoteza damu nyingi kupitia kwenye michubuko.
Wakati aina ya tatu dengue ni kupoteza fahamu, mgonjwa hupoteza damu nyingi ambayo husababisha apoteze fahamu na dalili hizi zimeonekana kwa mgonjwa mmoja kati ya wagonjwa 400 waliokwishathibitishwa kuwa na ugonjwa huo hapa nchini.
Jinsi ya kujikinga
Pallangyo anazitaja njia za kujikinga na ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kuangamiza mazalia ya mbu kwa kufikia madimbwi ya maji yaliyotuama, kunyunyuzia viatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo na kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalia ya mbu.
Nyingine ni kufyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu, kuhakikisha maua yanayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama, kufunika mashimo ya maji taka na kusafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama.
Kinga nyingine ni kujikinga na kuumwa na mbu kwa kutumia viatilifu vya kufukuza mbu, kuvaa nguo ndefu kujikinga na mbu, kutumia vyandarua na kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi.
Serikali inavyouzungumizia
Pallangyo anasema hadi sasa tayari ugonjwa huo umeua watu watatu Dar es Salaam na kusababisha jumla ya watu 460 kulazwa katika hospitali mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo, taasisi ya Magonjwa ya Binadamu(NIMR) iliyopo chini ya wizara ya afya, inaanza kufanya utafiti wa ugonjwa huu ili kujua ukubwa wa tatizo ambako inatarajiwa kuja na majibu hayo ndani ya mwezi mmoja.
Katika utafiti, Mkurugenzi wa NIMR, Dk. Mwele Malecela anasema utabainisha kujua jamii husika ya mbu wanaoambukiza ugonjwa huo, tabia ya kuuma watu, wapi wanapendelea kuuma, wapi wanakozaliana kwa wingi na mazingira yao ya kawaida.
Malecela anasema utafiti huo utaanzia Dar es Salaam na kuhusisha Wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni na baadye katika baadhi ya mikoa nane ambako vituo vya taasisi hiyo vipo na takwimu zitakazopatikana zitaweza kuboresha mbinu za kupambana na ugonjwa huu.
Katika kuhakikisha wanadhibiti ugonjwa huu, Pallangyo anasema wizara itaendelea kutoa taarifa ya tahadhari kuhusu ugonjwa huo kupitia kwa waganga wakuu wote wa mikoa sambamba na kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari na vipeperushi vinavyoeleza jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Pia ni katika kupambana na ugonjwa anawataka wadau mbalimbali wakiwemo Waganga wa Tiba Asili kwa mwenye taarifa yoyote ya utafiti wake kuhusu tiba ya ugonjwa huo kuipeleka wizarani ili kuona ni namna gani watashirikiana katika kuutokomeza ili usiendelea kuangamiza Watanzania.
Kwanini upo Dar es Salaam tu?
Mganga Mkuu, Donan Mbando anasema sababu ya ugonjwa huu kuwepo Dar es Salaam inatokana na kukithiri kwa uchafu ukilinganisha na mikoa mingine.
Mwishoni mwa iliyopita Nabii Yaspi Bendera wa kanisa la Ufunuo, Yombo,aliyetabiria ugonjwa huo aibuka na kuwakumbusha waumini namna alivyotabiri miezi mitatu iliyopita kuibuka kwa ugonjwa wa ajabu ambao alidai utaua madaktari na watu maarufu lakini akapuuzwa.
Katika ibada hiyo pia aliweza kumuombea mtu mwenye ugonjwa huo aliyejitambulisha kwa a jina la Godwin Emmanuel(48), ambaye alitoroshwa hosptalini na ndugu zake akiwa na sindano za drip mkononi na baadaye kumtaka kurudi hospitalini kutolewa sindano hizo kwa madai yeye sio mtaalam wa kuzitoa.
Via:Tanzania Daima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni