Kurasa

Alhamisi, 17 Aprili 2014

TWENDE KWA PILATO!

Thursday, April 17, 2014
KAIMU MKURUGENZI TANESCO KIZIMBANI KWA MATUMIZI MABAYA YA OFISI
Na Miriam Mosses
Aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Robert Semtutu na wenzake wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashitaka mawili ikiwemo kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh.milioni 200.
Washtakiwa wengine ni, aliyekuwa Afisa Ugavi wa Tanesco, Hanin Mahambo, Mkurugenzi wa fedha Lusekeo Kasanga,Mwanasheria Godson Ezekiel pamoja na Mkandarasi Martin Abraham.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Isidori Kyando alidai kuwa washtakiwa walifanya makosa hayo katika tarehe tofauti mwaka 2011.
Kyando alidai kuwa shitaka la kwanza ni la matumizi mabaya ya Madaraka, Desemba 2011,katika ofisi za Tanesco Ubungo, jijini Dar es Salaam washtakiwa kwa pamoja walitumia madaraka yao vibaya kwa kufanikisha malipo kwa msambazaji M/S Young Dong Electronic Co Ltd bila kuhakikisha kwamba Mkandarasi anafika katika kituo cha mwisho. Ilidaiwa kuwa washtakiwa walifanya kosa hilo kinyume na kifungu namba 35 (21) cha sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 na kusababisha Martin Abraham kupata faida kutokana na ukandarasi huo. Katika shitaka la pili ni la kuisababishia serikali hasara linalowakabili mshtakiwa Semtutu, Mahombo,Kasanga na Ezekiel ambao wanadaiwa kwamba kati ya Januari hadi Desemba 2011 katika ofisi za Tanesco Ubungo waliisababishia serikali hasara ya Sh.275,040,000 kutokana na matumizi yao mabaya ya madaraka.
Washtakiwa wote walikana kutenda kosa hilo ambapo upande wa mashitaka ulidai kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe nyingine ya kuwasomea washitakiwa hao maelezo ya awali.
Hakimu aliwaeleza washitakiwa hao kwamba dhamana yao iko wazi ikiwa watajidhamini wenyewe kwa kuwasilisha mahakamani hapo fedha taslim Sh.milioni 27.5 au kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika.
Pia wawe na wadhamini wawili kila mmoja watakaoweka ahadi ya dhamana ya kiasi icho cha fedha.
Hata hivyo wadhamini hao hawakutimiza masharti na wamerudishwa rumande hadi Aprili 30, mwaka huu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni