Kurasa

Jumanne, 22 Aprili 2014

POLE SANA WA JAJI!

Kwanini JK amemtoa kafara Jaji Warioba?
WAHENGA wanasema rafiki yako ndiye adui yako. Wengine wakasema akumulikaye mchana usiku atakuchoma. Hivi ndivyo alivyofanyiwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Jaji Warioba amekejeliwa na kutukanwa matusi ya kila aina kutoka kwa baadhi ya wanachama wa CCM na viongozi wao, wasomi na malofa kadhaa ambao hata shule yao inatiliwa shaka.
Sasa kile kinachotia shaka, watukanaji hao hawamtazami Jaji Warioba kama mwenyekiti aliyeongoza kundi la watu 30, isipokuwa wanamwandama kana kwamba mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu yao ni yake binafsi kutoka mfukoni mwake.
Haya ni matusi makubwa sana ya udhalilishaji wa hali ya juu kwa kiongozi aliyetukuka kama Jaji Warioba. Bahati mbaya sana wengi wanaoendelea kumtukana wamelishwa matusi pasipo hata kuisoma rasimu ya tume na viambatanisho vyake wakaona msingi na sababu za kile walichokipendekeza.
Kwa msingi huu ni lazima tumuulize na kumlalamikia Rais Jakaya Kikwete kwamba ni kwanini amekubali kumtoa kafara Jaji Warioba hadi anatusiwa na vifaranga?
Rais Kikwete ndiye aliunda tume na kumteua Jaji Warioba kuwa mwenyekiti. Hakushinikizwa na mtu katika uteuzi huo, anamfahamu aliyemteua kuwa ni muumini mtiifu wa CCM na msimamo wake aliuelewa, lakini amekuwa wa kwanza kufungua mlango wa kumdhalilisha na tume yake.
Hivi huyu mzee wa watu amekosea nini hadi amefikishwa hatua hiyo? Narudia tena kwamba bado namlaumu Rais Kikwete kwa hili, maana muda wote wa utawala wake ameonekana kuwajali na kuwaheshimu wazee kwa ushauri, lakini sijui Jaji Warioba alimfanya nini?
Wote tunakumbuka jinsi CCM ilivyomshurutisha Jaji Warioba hadi kulazimishwa kuwasilisha rasimu yake kabla ya rais kulizindua Bunge la Katiba. Huu ulikuwa uvunjwaji mkubwa wa kanuni za Bunge, lakini Jaji Warioba alikuwa mtiifu.
Rais anajua kwamba Jaji Warioba aliwasilisha rasimu kwa wajumbe wa Bunge ambalo kimsingi lilikuwa halijaanza kazi rasmi, lakini bado akamkejeli na kumdhalilisha siku alipolizindua Bunge na kudai kwamba takwimu zao kuhusu watu waliohojiwa juu ya muundo wa muungano hazina mashiko.
Kikwete alimtoa kafara Jaji Warioba, na hivyo kufungua ukurasa wa matusi kwa kila mtu pale aliposema kuwa mapendekezo yao ya muundo wa serikali tatu hayatekelezeki.
Kwa ujasiri wa hali ya juu pasipo kujua anajiumbua mwenyewe, Kikwete alisema kuwa Serikali ya Shirikisho inayopendekezwa inaelea tu, rais wake hana mamlaka, hana ardhi, hana rasilimali, hana uwezo wa kukopa na hivyo hatakuwa na uwezo wa kulipa mishahara ya majeshi yake, kwamba upo uwezekano majeshi hayo yakapindua serikali za washirika wake endapo hawatachangia fedha.
Kauli hii ilikuwa mbaya, tatanishi, vitisho, hofu na ndiyo imeibua upuuzi unaoendelea sasa wa kila kiongozi wa CCM na wajumbe wake bungeni kueneza uongo, kwamba serikali tatu zitaleta vita na kumzushia kila baya Jaji Warioba.
Ama kweli akutukanaye hakuchagulii tusi. Baada ya rais kuidhalilisha tume aliyoiteua mwenyewe ikamletea ripoti aliyoipokea na kuikubali ikabidhiwe kwa Bunge Maalumu kuendelea na mchakato, ameivunja Tume ya Warioba kimya kimya kwa kushtukiza, wajumbe wakanyang’anywa magari na ofisi bila kuambiwa, na sasa tovuti ya tume nayo imefungwa ili wananchi wasifanye rejea ya kile walichopendekeza.
Kwa mtu makini, kila ukimaliza kusoma mstari mmoja wa andiko hili unapaswa kujiuliza ni kwanini awe Jaji Warioba pekee? Mbona tume hiyo walikuwemo watu wengine mashuhuri wenye heshima zao kama Joseph Butiku, Salim Ahmed Salim, Prof. Mwesiga Baregu, Prof. Palamaganda Kabudi, hayati Dk. Sengondo Mvungi, Jaji mstaafu Augustino Ramadhani na wengine?
Hata walipolalamika kunyang’anywa magari na ofisi kinyemela huku tume ikivunjwa kabla ya tangazo la serikali kutolewa gazetini, Ikulu iliibuka na matusi ya hovyo hovyo kwa Mzee Warioba ikimwita mnafiki! Kweli Jaji Warioba kwa mtazamo wa Ikulu ni mnafiki? Sasa ebu tujiulize Rais Kikwete ikiwa alifahamu unafiki wa Warioba, alimteuaje kuwa mjumbe wa tume nzito kama hiyo na tena kuwa mwenyekiti? Mnafiki aliwezaje kuleta mapendekezo ya wananchi rais akayapokea na kuyakubali yaende kujadiliwa na Bunge la Katiba? Kwanini kama Ikulu iliona serikali tatu ni hatari na nchi inaweza kupinduliwa na majeshi iliyakubali halafu leo iseme Jaji Warioba ni mnafiki?
Kwa viongozi waliostaharabika, kwa hatua ambayo Jaji Warioba amefikishwa akitukanwa na CCM, Rais Kikwete kama mteule wake alipaswa kujitokeza na kutoa neno la ufafanuzi pamoja na kumtia faraja mzee wetu hata akishindwa kuomba radhi ya moja kwa moja kwake, lakini angalau atajiepusha na laana ya milele kwa sababu matusi haya wanatukanwa wananchi waliotoa maoni yao kwa tume.
Tumewasikia CCM, tena kupitia mtoto wa muasisi wa taifa hili, Mfaume Kawawa, aitwaye Zainab Kawawa, akisema uzushi bungeni kwamba Tume ya Jaji Warioba ina ajenda ya siri na wapinzani, hususani CHADEMA, kwa sababu ilikusanya maoni kwenye maeneo yanayoongozwa na chama hicho.
Turudi kwenye swali letu la kwanini Kikwete amemtoa kafara Jaji Warioba? Je, ni kweli Jaji Warioba anataka muungano uvunjike na nchi isiwe na utulivu? Hawa wanaosema hivyo wanafahamu historia ya muungano ama wanasherehesha tu propaganda zao? Hivi wanajua kwamba wanamtukana rais wao ambaye alimtuma Jaji Warioba au wanabwabwaja tu?
Ukiachilia mbali wasomi kadhaa walioamua kulamba matapishi yao na kumtusi Jaji Warioba na wana-CCM wengi wanaotukana bila kujua wanamtusi nani, katikati yake utaona wanaosalia si bure wana jambo na sababu za kufanya hivyo, hawa bila shaka wanalipa kisasi.
Ikumbukwe kwamba mwaka 1997, Jaji Warioba aliongoza Tume ya Rais Benjamin Mkapa iliyochunguza na kubainisha mianya na vyanzo vya rushwa nchini. Japokuwa ripoti hiyo iliwekwa kabatini, lakini wako vigogo kadhaa waliguswa na wengi wao ndio hao walioshika madaraka leo.
Hawa wanawezaje leo kumsifu Jaji Warioba wakati alishaharibu kitumbua chao? Hatuoni huu ndio mwanya wao wa kutaka kumdhoofisha wakati huu hata wengine wakijipanga kuwania urais wa nchi ili kuficha madhambi yao yaliyomo kwenye ripoti ya rushwa 1997?
Sasa CCM wametunga uongo mwingine kwamba waasisi wa taifa hili; hayati Julius Nyerere na Abeid Amani Karume wametukanwa huku wakifahamu fika serikali yao ndiyo ilikumbatia hati za muungano bila kuzionyesha.
Eti naye Rais Kikwete ameibuka akionya kwamba wazee hao waheshimiwe, lakini haguswi na matusi ya wazi wazi kwa Jaji Warioba, kulikoni? Tafakari!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni