Kurasa

Jumamosi, 26 Aprili 2014

KWELI PALIPO NA WAKUBWA HAPAHARIBIKI JAMBO.KINGUNGE ADHIHIRISHA UTU UZIMA WAKE.

MWANASIASA mkongwe na Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Kingunge Ngombale – Mwiru, amesema makada wenzake wanaomshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, wanakitukana Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kumtukana au kumshambulia Jaji Warioba, au wajumbe wengine wa tume hiyo ni sawa na kukitukana Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza serikali.
Kingunge alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akichangia sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya Katiba, ambapo alisema wanaomshambulia Jaji Warioba wanaonyesha utovu wa adabu, kwa kuwa chama kina maadili na adabu katika kushughulikia masuala mbalimbali.
“Mimi sitakubali hata kidogo wajumbe watumie msimamo wa chama kumshambulia Warioba au wajumbe wengine wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, si halali kumshambulia Warioba au mjumbe yeyote yule binafsi.
“Mimi ni Mwana CCM niliyeondoka madarakani siku nyingi lakini naamini kuwa kumtukana mwenzetu ni sawa na kukitukana chama na sisi tuliopo hapa, wanaomshambulia Warioba wanakosea sana, hapa tuna rasimu ya Katiba ambayo ina mawazo tu, hakuna watu ndani ya rasimu hiyo, hatupaswi kukiuka maadili kwa kuwatukana au kuwakashifu watu,” alisema.
Alisema kilichomo ndani ya rasimu ya Katiba si uamuzi wa mwisho, hivyo wajumbe hawana sababu ya kumsema, kumtukana au kumkejeli mtu yeyote aliyekuwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Kingunge pia alitumia fursa hiyo kukemea lugha za matusi, vijembe na kejeli zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wajumbe kwenye mijadala mbalimbali.
“Hatuwezi kukaa hapa ndani kwa kudhalilishana, wale waliokuwa wakitumia lugha hizo walikuwa wanatudhalilisha wote. Wengine walitumia lugha hizo kwa waasisi wetu…Unyenyekevu ni sura moja ya msomi ambaye ametumia fedha za Watanzania kupata elimu yake,” alisema.
Alisema wajumbe wamekwenda bungeni kuwatafutia wananchi wenzeo Katiba mpya, iliyo bora na lazima izingatie miaka 50 ya muungano ambao umekuwa na mafanikio makubwa.
“Katiba bora lazima iimarishe yale mafanikio tuliyoyapata katika kipindi hicho ikiwemo muungano, umoja wa kitaifa, mshikamano, udugu na kuunda mazingira ya amani na utulivu, kama haiimarishi, haifai hata kidogo. Haya mafanikio yote yametokana na muundo wa serikali mbili ulioasisiwa na wazee wetu,” alisema.
Hakuna Katiba bila UKAWA
Kingunge alisema kuwa ili Tanzania ipate Katiba mpya iliyo bora, lazima kuwepo maelewano ya kuwashirikisha wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Alisema kitendo cha wajumbe wa UKAWA kususia vikao vya Bunge, kinaonyesha upungufu mkubwa walionao lakini Katiba mpya haitaweza kupatikana bila ya wao.
Kingunge aliwaomba wajumbe wa UKAWA warejee bungeni kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa Katiba ya wananchi.
Alisema hata UKAWA wakirejea bungeni ni vema wajumbe wakatambua kuwa kupatikana kwa Katiba mpya kunahitaji maridhiano ya pande hizo mbili.
“Hatuwezi kupata theluthi mbili ya kura hasa kwa wajumbe wa kutoka Zanzibar watakaohalalisha maamuzi yetu bila kushirikiana na wenzetu, lazima tuzungumze, theluthi mbili ni takwa la kisheria, hatuwezi kulikwepa,” alisema.
Kingunge alisema kwa muda mrefu Zanzibar kulikuwa na mfarakano mkubwa kati ya CCM na CUF lakini yalifanyika mazungumzo yaliyodumu kwa takriban miaka 13.
“Tumezungumza kwa muda mrefu tangu 1998 lakini hatimaye tulibuni suala la kugawana madaraka…katika hali ya Zanzibar tulisema haiwezekani lazima tukubaliane, sasa Zanzibar imetulia. Ni kutokana na mazungumzo hayo.
“Suala la Katiba mpya si utani ni lazima tukubali tuzungumze mpaka tuelewane….humu ndani sisi wajumbe tuzungumze lakini na wakubwa huko nje nao ni lazima wazungumze,” alisema.
UKAWA waliteka Bunge
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Alli Idd, wamewataka wajumbe wa UKAWA wabatilishe uamuzi wa kususia vikao vya Bunge Maalumu.
Kauli hizo walizitoa jana walipokuwa wakichangia sura ya kwanza na ya sita za rasimu ya Katiba, ambapo walisema Katiba inayotungwa ni ya Watanzania wote, hivyo ni vema UKAWA wakarejea bungeni.
Balozi Iddi alisema taifa limetumia fedha nyingi kugharimia ujenzi wa Bunge Maalumu pamoja na kuwagharimia posho wajumbe wake ambapo mpaka jana lilitumia zaidi ya sh bilioni 20, hivyo si busara kwa UKAWA kususia vikao.
Alisema UKAWA ni sehemu muhimu katika utungaji wa Katiba na wajumbe wake wametumwa na wananchi ambao wanataka matatizo yao yawekewe utaratibu wa kushughulikiwa kwenye Katiba.
Alisema kutokana na umuhimu wa kutunga Katiba, Rais Jakaya Kikwete, amekubali kuliongezea muda wa siku 60 zaidi Bunge hilo ambalo jana limeahirishwa hadi Agosti 5, mwaka huu.
Alisema kuongezewa siku huko kumetokana na kutokamilisha kazi yake kwa siku 70 zilizopangwa awali ambazo zimemalizika jana hivyo UKAWA wanapaswa kutambua unyeti wa vikao vya bunge na umuhimu wao.
“Pamoja na serikali kutumia fedha nyingi kutengeneza ukumbi na kulipana posho UKAWA wameamua kususia vikao vya Bunge. Nawasihi warudi tuendelee na kazi hii tuliyopewa na wananchi. Katiba haitungwi barabarani au kwenye mikutano ya hadhara bali bungeni.
“Nawasihi warejee bungeni tuifanye kazi hii tuliyotumwa na wananchi, tumetumia fedha nyingi na tutaendelea kutumia, kila mmoja wetu analipwa sh 300,000 kwa siku na serikali inatumia sh milioni 188 kwa siku kulipa posho.”
Naye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema anaamini katika umoja, hivyo kukosekana kwa wajumbe wa UKAWA ndani ya Bunge kumemsikitisha lakini ataendeleza jitihada za mazungumzo nao.
Pinda ametoa rai hiyo wakati ni takriban wiki moja imepita tangu alipokaririwa akitamba kuwa wanawafuata UKAWA huko huko kwa wananchi kwenda kusema ukweli.
Pinda aliwasihi wajumbe wa UKAWA warejee bungeni huku akiwasihi wajumbe wengine wajiepushe na lugha za kejeli na vijembe ambazo alidai zimechangia mijadala kuwa katika mazingira magumu.
‘Mimi kila siku huwa nasema kuwa yaliyopita si ndwele…tugange yajayo, naomba wenzetu UKAWA warejee bungeni, Katiba mpya inahitaji ushirikiano wetu sote,” alisema.
Pinda pia alisema Tume ya Jaji Warioba imefanya kazi nzuri kwa kuwa yapo mambo mengi ambayo hayamo kwenye Katiba ya sasa lakini yameorodhoshwa kwenye Rasimu ya Katiba.
Alibainisha kuwa anapingana na rasimu hiyo katika eneo moja la muundo wa serikali tatu kwa kuwa anaamini ni mzigo mkubwa kwa taifa na litachangia kuvunja muungano.
Alisema kuwa wanaosema kuwa kutofuata mapendekezo ya tume ya Warioba kwa kuwa imetumia fedha nyingi, wanakosea kwani wajumbe wa Bunge Maalumu wamepewa fursa ya kuondoa, kuboresha na kuingiza mawazo wanayoona yanafaa kuwemo kwenye Katiba mpya.
Naye Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, alisema kiti chake kiliamua kuwaacha wajumbe wajadili kwa uhuru zaidi na wananchi waamue kipi kinafaa.
‘Huko mitaani tunalaumiwa kwa kuwaachia wajumbe, sisi tulifanya hivyo pasipo kutumia nguvu, kanuni au askari ili wananchi wajue tabia za wajumbe wao na kuamua, tungebanana sana najua lazima tungepigana na kutoana ngeu,” alisema.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni