Kurasa

Jumamosi, 19 Aprili 2014

KAMA UNATAKA AJIRA SERIKALINI HIZI HAPA SOMA MALA MOJA UCHUKUE HATUA.

. Katika kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini mwaka huu, Serikali inatarajia kuajiri wafanyakazi wapya zaidi ya 11,000, imeelezwa.
Taarifa hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen Kebwe wakati wa kufunga Mradi wa Maisha unaoendeshwa na Taasisi ya Jhpiego chini ya udhamini wa Mfuko wa Misaada wa Marekani (USAID).
Dk Kebwe alisema pamoja na kuwa Tanzania inapiga hatua katika kuboresha huduma ya afya, bado kuna changamoto kadhaa zikiwapo za upungufu wa wafanyakazi na kushindwa kufikia baadhi ya malengo ya milenia yanayotakiwa kukamilika mwaka 2015.
Alisema ni mara ya kwanza katika historia ya sekta hiyo nchini kuajiri wafanyakazi wapya 11,221 kwa wakati mmoja.
“Hii ni idadi kubwa kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kuajiri wafanyakazi wengi,” alisema.
Mgeni rasmi katika mkutano huo, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal alisema Tanzania imepunguza idadi ya vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutokana na michango ya mashirika mbalimbali ya kimataifa.
Huku akiumwagia sifa Mradi wa Maisha ambao upo nchini kwa miaka mitano, Dk Bilal alisema mradi huo umetoa huduma za afya katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Maisha kwa kushirikiana na Serikali wamefanikiwa kuwekeza vitega uchumi muhimu ambavyo vitatuletea matokeo chanya katika majibu ya utafiti yatakayotolewa baadaye kutoka kupunguza vifo vya wajawazito 454 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2010,” alisema Dk Bilal.
Pia alisema kuwa ripoti iliyotolewa mwaka jana na Umoja wa Mataifa kuhusu vifo vya watoto, ilionyesha kuwa Tanzania imefanikiwa kutimiza lengo namba nne kwenye maendeleo ya milenia kwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
“Matokeo hayo yanatokana na kuongeza udhibiti wa malaria, utoaji wa Vitamini A na udhibiti wa magonjwa ya watoto,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Maisha, Dk Dunstan Bishanga alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani ambazo zina vifo vya wajawazito kwa zaidi ya asilimia 60.
Kuhusu vifo vya watoto wanaozaliwa, Dk Bishanga alisema kuwa lengo namba nne la MDG ni kupunguza vifo hivyo hadi asilimia 46 ifikapo 2015, lakini hadi sasa Tanzania ina asilimia 68.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni