Kurasa

Jumamosi, 19 Aprili 2014

HISTORIA YA PASAKA

Wakristo duniani kote wanajiandaa kusherehekea Sikukuu ya Pasaka. Ingawa si madhehebu yote ya Kikristo yanayosheherehea kwa uzito sawa, katika kalenda ya Kanisa Katoliki, Pasaka ni furaha ya kusherehekea kufufuka kwa Yesu.
Ijumaa Kuu
Ijumaa Kuu ni siku ambayo wakristo wanaadhimisha kufa, kuzikwa kwa Yesu, tukio lililotokea katika mji wa Yerusalemu siku ya Ijumaa.
Kulingana na Mtume Yohane, kesho yake, yaani baada ya Ijumaa, ilikuwa Sabato na ikafuatia na Pasaka yenyewe siku ya Jumapili. Ijumaa Kuu ni sehemu ya Juma Kuu linaloanza kwa adhimisho la Yesu kuingia mji huo wa Yerusalemu akishangiliwa kama mfalme wa Wayahudi. Ijumaa Kuu pia ni sehemu ya siku tatu kuu za Pasaka zinazoadhimisha mateso na kifo chake, kuzikwa kaburini, na hatimaye kufufuka.
Umuhimu wa Pasaka
Pasaka ni moja ya sikukuu kubwa sana kwa Wakristo. Pamoja na kuwa imeendelea kuchukuliwa kama tukio la kihistoria tu, bado dhana yake ya kuonyesha upendo wa Mungu kwa wanadamu haitapotea. Ni upendo wa kutoa moja ya nafsi za Mungu, iteswe, isulubiwe, ife na kisha ifufuke kudhihirisha utukufu wa Mungu na upendo wake kwa wanadamu.
Lakini kwa sisi wanadamu wa leo Pasaka ni nini?
Kuna umuhimu gani wa kuendelea kukumbuka Sikukuu ya Pasaka? Ni mafundisho gani tunayoyapata juu ya siku hii? Pasaka ni sikukuu ya kufufuka kwa Yesu Kristo na ni sikukuu muhimu kwa Wakristo, watu huenda kanisani na kusherekea sikukuu hii ya kidini.
Wakristo pote ulimwenguni husherekea Pasaka kwa furaha kubwa sana kwa sababu wanaiona ndio siku ambayo mwokozi wao huwa amefufuka. Watu wengi huvalia nguo mpya kwenda kanisani siku ya Pasaka.
Kuna alama nyingi zinazotambulisha siku ya Pasaka, moja ni msalaba ambao Wakristo, huuona kama alama ya ushindi wa Kristo dhidi ya kifo. Msalaba mara nyingi hutokea kama alama ya Pasaka. Watu katika sehemu nyingi ya ulimwengu huoka keki maalumu ziitwazo 'mikate ya moto ya msalaba'.
Mishumaa
Taa, mishumaa na moto mkubwa wa sherehe inatoa ishara ya kusherekea kwa Pasaka katika baadhi ya nchi.
Wakatoliki katika baadhi ya nchi huzima taa zote katika makanisa yao siku ya Ijumaa kuu. Jioni ya siku inayotangulia Pasaka, hutengeneza moto mpya kuwashia mshumaa mkubwa wa Pasaka kuashiria siku na mambo mapya ndani ya ufufuo mpya wa Yesu.
Hutumia mshumaa huu kuwashia mishumaa mingine yote kanisani. Halafu huwasha mishumaa yao nyumbani ili itumike katika nyakati za sherehe maalumu.
Katika sehemu za Ulaya Kaskazini na Kati,watu huchoma moto mkubwa wa sherehe katika vilele vya milima. Halafu hujikusanya kuzunguka huo moto mkubwa na kuimba nyimbo na mashairi ya Pasaka.
Mwanzo wa Pasaka
Wakristo hufanya ibada ya siku 40; kipindi cha mfungo na sala hujulikana kama Kwaresma.Inakumbusha siku 40 za Kristo kufunga na kwenda jangwani.
Wiki ya mwisho ya Kwaresma iitwayo wiki takatifu hutukuza matukio ya wiki ya mwisho wa maisha ya Yesu Kristo kuwepo duniani, na inaanza katika Jumapili ya Matawi. Imetajwa hivyo kwa sababu ya matawi ambayo watu waliyatawanya kabla Yesu kristo hajaingia Yerusalemu kwa kushangiliwa
kwa shangwe kubwa.
Katika Alhamisi ya wiki ya mwisho ya Kwaresma kabla ya Ijumaa Kuu, Wakristo hukumbuka chakula cha mwisho cha Yesu Kristo cha jioni wakati walipoosha nyayo za miguu yao.
Waliiona Ijumaa Kuu ya kusulubiwa kwa Yesu kristo katika namna au njia ya huzuni na majonzi na kutumia Jumamosi takatifu katika fikra ya mambo yatakayotokea mbeleni katika Jumapili ya Pasaka. (FRIDAY SIMBAYA)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni