Kurasa

Jumatano, 23 Aprili 2014

GHASIA AONGOZA MZISHI YA CHANG'A.

.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi), Hawa Ghasia jana aliongoza mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, Moshi Chang’a yaliyofanyika katika makaburi ya Mtwivila, Kihesa Iringa.
Akizungumza katika mazishi hayo, Ghasia alisema Chang’a alikuwa mchapakazi na kuwa hata yalipofanyika mabadiliko ya maeneo ya kazi kutoka wilaya moja kwenda nyingine, hakuwahi kulalamika tofauti na ma-DC wengine.
Alitoa pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa wilaya aliyokuwa akiiongoza kwa kuondokewa na mchapakazi huyo.
Ghasia aliwataka wananchi wakati wote kuwa tayari kwa kifo na kutenda mema kwa watu wote bila kujali itikadi zao za kisiasa na kidini, kama alivyokuwa Chang’a.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya alisema DC Chang’a alikufa kutokana na shinikizo la damu na kisukari, na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu Machi 29, mwaka huu.
Alisema wakati wa uhai wake, marehemu Chang’a alikuwa mcheshi na mchapakazi kwa jamii anayoitumikia.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema Chang’a ndiye aliyechangia yeye kupata wadhifa huo alionao.
Spika Makinda alisema alipata ubunge wa Njombe Kusini mwaka 1995 katika uchaguzi wenye ushindani mkali na wa kwanza wa vyama vingi kwa msaada mkubwa kutoka kwa Chang’a, wakati huo akiwa Katibu wa CCM Wilaya ya Njombe.
Alisema Chang’a alifanikisha masuala mengi ambayo yaliwashinda watu wengi, ikiwamo kutuliza vuguvugu la kisiasa na kuwasikiliza watu wote bila kujali itikadi za kisiasa na kidini.
Alisema licha ya kushinda kwenye uchaguzi huo katika ushindani mkali wa NCCR-Mageuzi, baadaye ilifunguliwa kesi ambayo ilidumu kwa miaka minne na mmoja wa waliosaidia kushinda kesi hiyo ni Chang’a.
Alisema ni vyema kuiga mfano wa utendaji wa kiongozi huyo hasa kwa kuweka mbele masilahi ya Taifa.
Meneja wa Wakala wa Misitu Kanda ya Kusini, Bruno Mallya alisema enzi za uhai wake, marehemu alihimiza wananchi kutunza mazingira.
KUTOKA MWANANCHI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni