Kurasa

Jumatano, 22 Aprili 2015

MWANAFUNZI ATANDIKWA VIBOKO NA WALIMU MPAKA KUFA KITETO


Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Matui wilayani Kiteto, amefariki dunia darasani baada ya kudaiwa kuchapwa viboko na walimu watatu wa shule hiyo, kwa kile kilichodaiwa kufeli mtihani wa Kiswahili.

Polisi wilayani na mkoani Manyara, wanamshikilia mwalimu mmoja baada ya wenzake kukimbia baada ya tukio.

Akizungumza jana, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Kanali Samwel Nzoka alimtaja mwanafunzi huyo aliyepoteza maisha kuwa ni Noel Bichima (15).

Kanali Nzoka alisema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi wakiwa darasani, wakati mwalimu huyo anayeshikiliwa na polisi alipokuwa akiwafundisha. Inadaiwa mwanafunzi huyo alichapwa viboko vinane. Haikuelezwa kama alichapwa kiganjani ama sehemu nyingine.

Nzoka alidai kuwa mwalimu huyo alimchapa marehemu baada ya kupata alama 40 katika mtihani wa somo la Kiswahili kwani walipeana mkakati wa kutofeli na kwamba mwanafunzi atakayepata chini ya alama 40 atachapwa fimbo 12.

“Mwanafunzi huyo alifariki dunia papo hapo darasani baada ya kuanguka chini alipochapwa viboko na walimu hao na mwili wake umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kiteto ukisubiri uchunguzi,” alisema Kanali Nzoka.

“Natoa wito kwa walimu wa shule za msingi na sekondari, kuangalia namna ya kutoa adhabu kwa wanafunzi wanapokosea, baadhi ya watoto afya zao siyo nzuri,” alisema Kanali Nzoka.

Diwani wa Kata ya Matui, Athumani Kidawa alisema baadhi ya wazazi wa eneo hilo waliopatwa na hasira baada ya kutokea tukio hilo, waliandamana hadi Kituo cha Polisi Matui kulalamikia kitendo hicho.
MPEKUZI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni