Kurasa

Jumatano, 8 Oktoba 2014

WATUMISHI MAFIA WAHUKUMIWA KWA UFISADI

Mafia. Mahakama ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani imewatia hatiani na kuwahukumu kifungo cha miaka minne jela au faini ya Sh3 milioni watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia baada ya kuridhika wametenda kosa la ubadhirifu wa Sh7.5 milioni zilizokusudiwa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Watumishi hao watatu ni William Kimaro aliyekuwa ofisa utumishi, Geofrey Kiwelu (mweka hazina) na Hatibu Kwao Amanzi aliyekuwa mtunza fedha.
Kila mmoja alitakiwa kulipa fedha hizo au kutumikia adhabu hiyo.
Akisoma hukumu hiyo, hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mafia, Hassan Makube alimtia hatiani Geofrey Kiwelu kwa kosa jingine la kuharibu nyaraka kinyume na kifungu cha 109 cha sheria ya kanuni za adhabu na kumhukumu kwenda jela miaka mitatu au faini ya Sh1 milioni.
Hukumu ya kesi hiyo iliyokuwa na makosa 12, iliwaona hawana hatia na kuwaachia huru watumishi wengine watatu ambao ni William Zakaria Shimwela, Lusasi na ofisa mipango, Brenden Oswin Kachenje.
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, John Sang’wa aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa waliotiwa hatiani ili iwe fundisho kwa watumishi wengine.
Mwananchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni